ASKOFU MOKIWA AKUBALI YAISHE,AIFUTA KESI YAKE MAHAKAMANI,SOMA HAPO KUJUA
Aliyekuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana Jimbo
la Dar es Salaam, Valentino Mokiwa, amewasilisha barua mahakamani akiomba
kuondoa kesi aliyoifungua akipinga kustaafishwa kwa nguvu ili wakamalizane
katika nyumba ya maaskofu.
Mokiwa anataka kuondoa kesi hiyo ya madai namba 20
ya mwaka huu aliyofungua dhidi ya Askofu Mkuu wa Makanisa ya Anglikana
Tanzania, Mhashamu Dk. Jacobe Chimeledya na Bodi ya Wadhamini ya kanisa hilo.
Askofu Mokiwa alifungua kesi hiyo katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu na iko mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Akiieleza mahakama, Wakili wa wadaiwa, Gabrieli
Masinga alidai alipokea barua kutoka kwa Wakili wa Askofu Mokiwa, Wakili
M.B. Kabunga ikiwaelekeza kuwa kesi iliitwa jana kwa sababu waliwasilisha barua
ya kuomba kuiondoa mahakamani.
Alidai barua hiyo ilieleza sababu za kuondoa kesi
hiyo ni kutokana na juhudi za kutatua mgogoro huo katika nyumba ya maaskofu.
“Wanaomba kuondoa kesi wapate muda
wa kujadiliana kwa sababu juhudi haziwezi kufanyika bila kesi hiyo
kuondolewa mahakamani,”alidai.
Hakimu Simba alisema barua hiyo hajaiona na kesi
hiyo ilipangwa Februari 28 hivyo kuwapo kwao jana mahakama hakutambui.
“Leo mliitwa na nani, mimi siandiki
kitu, niandike ili iweje, siwahitaji, kesi imepangwa tarehe 28, pisheni wengine
waendelee. Naona kuna barua ya kumalizana katika nyumba ya maaskofu, kama
ni hivyo nawaombea usuluhishi mwema,”alisema Hakimu Simba.
Askofu Mokiwa na wakili wake wote hawakufika
mahakamani. Hata hivyo Wakili Masinga alidai askofu huyo anataka
kurejeshewa uaskofu wake, anaomba mahakama itengue uamuzi wa kumstaafisha
kwa nguvu.
“Mokiwa alivuliwa uaskofu wake na
Januari 7 mwaka huu akakimbilia mahakamani, mambo yanayohusu imani yanatakiwa
kushughulikiwa katika nyumba za imani.
“Huwezi kuvuliwa madaraka msikitini ama
kanisani ukakimbilia mahakamani, masuala hayo yanajadiliwa katika vyombo husika
labda pakiwapo ukiukwaji wa sheria za nchi,”alidai.
Kwa mujibu wa barua kwa mapadri na maaskofu wote wa
Kanisa la Anglikana Jimbo la Dar es Salaam, kiongozi huyo alilazimishwa
kuvuliwa uaskofu Januari 7 mwaka huu.
Sababu za kuvuliwa madaraka kwa kiongozi huyo wa
muda mrefu wa kanisa hilo ni kudaiwa kuhusika na ufujaji wa mali za
kanisa na matumizi mabaya ya madaraka.
Inadaiwa katika hati kwamba hatua hiyo inatokana na
mashtaka yaliyowasilishwa dhidi yake na wadhamini wa makanisa mbalimbali ya
Jimbo la Dar es Salaam, ambayo ni Yombo Buza na Magomeni ambao
walilalamikia matumizi mabaya ya madaraka kwa kile walichoita ufisadi
huku wakimtaka aandike barua mwenyewe ya kujiuzulu lakini aligoma kufanya
hivyo.
Mokiwa anakabiliwa na mashtaka 10 huku shtaka la
tatu la uwekezaji, ndilo lililomtia hatiani na yeye kukiri kosa mbele ya tume
hiyo ya uchunguzi.
Kesi hiyo itaendelea Februari 28 mwaka huu na
mahakama itaelezwa kama kuna makubaliano ya kuondoa kesi wakamalizane nje
ya mahakama au la.