Zinazobamba

UDOM NA UDSM KUTOKEA VURUGU,SAKATA LA MIKOPPO KWA WANAFUNZI LAFIKIA PABAYA,SOMA HAPO KUJUA

Prof. Rwekaza Mukandala, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ni vyuo ambavyo serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu hapa nchini (HESLB) inatarajia kuvinyima baadhi ya fedha za ada za wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2016/2017, anaandika Charles William.
Uamuzi wa kuvinyima fedha vyuo hivyo utachukuliwa ili kufidia upotevu wa fedha zinazofikia Sh. 650 milioni kutokana na uwepo wa wanafunzi hewa katika vyuo hivyo.
Prof. Simon Msanjila, Naibu Mkurugenzi wa Wizara ya Elimu, Mafunzo ya Ufundi amewambia wabunge wa Kamati ya Katiba na Sheria leo kuwa vyuo vilivyokutwa na wanafunzi hewa ambao walikuwa wakilipwa mikopo vimeitia hasara kubwa serikali na hivyo lazima viadhibiwe.
“Mpaka sasa serikali imekusanya Sh. 1.50 bilioni pekee kutoka katika vyuo vilivyokutwa na wanafunzi hewa huku UDSM na UDOM vikikutwa na idadi kubwa ya wanafunzi hewa.
“Tuliwaandikia barua kuwataka walipe au watoe maelezo juu ya walipo wanafunzi hao ambao tayari walikuwa wameshalipwa jumla ya Sh. 3.85 bilioni ilihali hawapo vyuoni,” amesema Msanjila.
Uamuzi wa serikali kukata fedha za ada za vyuo vikuu vilivyoshindwa kurejesha fedha zinazodaiwa kulipwa kwa wanafunzi hewa utavifanya vyuo hivyo, kukosa mamilioni ya fedha ambazo hutumika kuendesha shughuli zao za kila siku.
Kuhusu baadhi ya wanafunzi kukosa mikopo ingawa wana sifa, Msanjila amesema wanafunzi wengi wamekuwa wakijaza taarifa za uongo katika fomu zao za maombi na hivyo kufanya bodi ya mikopo iwanyime mikopo hiyo.
“Utakuta mwanafunzi, baba yake ni fundi vyuma lakini anajaza kwenye fomu kuwa ni mhandisi au mama yake labda ni mpika vitumbua lakini yeye anajaza kuwa ni mfanyabiashara. Sasa mwanafunzi kama huyo tutampaje mkopo asilimia mia moja?” amesema Msanjila.

Katika orodha ya wanafunzi hewa wa vyuo vikuu hapa nchini, iliyotolewa na waziri Joyce Ndalichako tarehe 27 Agosti mwaka huu, UDSM iliongoza kwa kuwa na wanafunzi hewa 350 ambao waliolipwa Sh. 703.4 milioni huku ikifuatiwa na UDOM iliyokuwa na wanafunzi hewa 364 waliolipwa Sh. 460.9 milioni.
Vyuo hivyo vilitoa maelezo juu ya wanafunzi hao kukosekana wakati wa uhakiki huku vikipewa fursa ya kuwatafuta ili wahakikiwe hata hivyo baadhi yao walikosekana kabisa, kwahiyo vyuo vitakatwa fedha za ada zinazofikia Sh. 650 milioni.
Fedha za ada wanafunzi hulipwa na HESLB kwa vyuo vikuu ikiwa ni sehemu ya mikataba ya wanafunzi wanaolipiwa na serikali. Fedha hizo hutumika kusaidia uendeshaji vyuo hivyo.