MAALIM SEIF AMSHUKIA IGP MANGU,NI KUHUSU LIPUMBA NA GENGE LAKE,SOMA HAPO KUJUA
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif
Sharif Hamad, atatua ofisini kwa kiongozi mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP),
Ernest Mangu, ili kumueleza mkakati wake wa kutua ofisini kwake, Buguruni
jijini Dar es Salaam, anaandika Pendo Omary.
Maalim anakwenda kwa IGP Mangu
kumueleza adhima yake ya kufika ofisi kuu ya chama chake kesho Ijumaa, majira
ya saa mbili asubuhi.
Hatua ya Maalim kutinga ofisini kwa IGP imetokana na
kitendo cha jeshi la polisi kumsindikiza Prof. Lipumba kurejea ofisini; kusaidia
uharibifu wa mali na kushambulia wanachama na wafuasi wa chama hicho.
Azma yake ya kwenda ofisini kwake kesho, inatokana
na ofisi hiyo kuvamiwa na aliyepata kuwa mwenyekiti wa chama hicho, Prof.
Ibrahim Lipumba na genge la wafuasi wake.
Prof. Lipumba aliyejiuzulu uenyekiti wa CUF, 6
Agosti mwaka jana na miezi 11 baadaye akatangaza kurejea katika nafasi yake,
amefukuzwa rasmi uanachama wa chama hicho Jumanne iliyopita na Baraza Kuu la
uongozi la Taifa (BKT), lililokutana Visiwani.
Hata hivyo, Prof. Lipumba, ameendelea kung’ang’ania
kuwa bado mwenyekiti halali wa chama hicho na msimamo wake huo, unadaiwa
kuungwa mkono na msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa watu waliokaribu
na Maalim Seif zinasema, kiongozi huyo amekwenda kwa IGP Mangu kumtaarifu kuwa
yeye na wabunge wa chama hicho, wamepanga kufika Buguruni kwa pamoja.
Anasema, “Maalim Seif anakwenda kumweleza IGP Mangu
kwamba, tayari kumekuwepo na viashiria vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na watu
wa Prof. Lipumba na kwamba chochote kitakachotokea, yeye na jeshi lake,
wanapaswa kubeba msalaba.”
Prof. Lipumba alijiuzulu uenyekiti karibu na
uchaguzi mkuu mwaka jana, akakimbilia nje ya nchi huku akidai hakufurahishwa na
Edward Lowassa kuwa mgombea urais chini ya mwavuli wa vyama vinne ikiwamo CUF.
Ukawa unaundwa na vyama vinne; Chadema, CUF,
NCCR-Mageuzi na National League for Democrats (NLD).
Hii ni mara ya pili tangu mfumo wa vyama vingi
urejee nchini, kukumbwa na “mbegu mbaya” ndani yake.
Mara ya kwanza ilikuwa pale Augustine Mrema, akiwa
mwenyekiti, alipojiapiza kufukuza wanachama thabiti ndani ya NCCR-Mageuzi.
Alishindwa. Alifukuzwa mwenyewe.