VIONGOZI WA DINI WAVUNJA UKIMYA WAITOLEA UVIVU SERIKALI,NI KUHUSU OPARESHINI KABAMBE YA UKUTA,SOMA HAPO KUJUA
SERIKALI na viongozi wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), wametakiwa kukaa chini kutafuta suluhu ya mvutano
unaoendelea kuhusu operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta)
ili kuepusha vurugu kutokea nchini maandamano hayo yatakapofanyika.
Rai hiyo ilitolewa na Taasisi ya Maridhiano
inayoundwa na viongozi mbalimbali wa dini jijini Dar es Salaam jana.
Lengo la taasisi hiyo ni kuishauri serikali na
kutafuta suluhu na viongozi wa Chadema walioanzisha operesheni hiyo.
Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Mchungaji Osward Mlay,
alisema ili kuepuka machafuko yanayoweza kutokea wakati wa kutekeleza
operesheni hiyo Septemba mosi, mwaka huu huku Jeshi la Polisi likisema
litauvunja Ukuta ni vyema pande zote mbili zikajadiliana na kupata
mwafaka.
"Hakuna jambo lililoshindikana
mezani. Sisi kama taasisi ya maridhiano, tunaiomba serikali ikae mezani na
viongozi wa Chadema ili kumaliza tofauti," alisema.
Mchungaji Mlay aliongeza kuwa sababu ya kuwashawishi
Chadema na serikali kufanya maridhiano ni kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha
amani ya nchi inadumu na kuondokana na dhana ya viongozi wa dini kutafuta
usuluhishi pindi machafuko yanapotokea.
Alisema wana jukumu la kuwashauri viongozi wote wa
serikali pale wanapohisi kunaweza kutokea uvunjifu wa amani na kwamba hawako
tayari kukaa kimya pindi wanapoona ishara ya vitendo hivyo kama lilivyo lengo
lao.
Mchungaji Mlay pia aliitaka Chadema kusitisha
maandamano waliyopanga kufanya na badala yake wakae mezani kuona namna
wanavyoweza kudai demokrasia kwa amani badala kutumia njia ya maandamano.
Pia alivishauri vyombo vya dola kuongoza nchi kwa
mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamiwa na Katiba ya nchi bila kukandamiza
demokrasia.
Alisema wananchi pia wanapaswa kuepuka vitendo vya
uvunjifu wa amani kama kufanya maandamano yasiyo na tija kwa taifa ili
kusitokee vurugu zinazoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Naye Sheikh Mohamed Hariri, alisema wanategemea
serikali na Chadema watatafuta suluhu badala ya kusubiri machafuko yatokee.