BAADA YA WATUMISHI HEWA SERIKALI YAHAMIA KWA WANAFUNZI HEWA,SOMA HAPO KUJUA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa
Wilaya na Maofisa Elimu nchini wafanye ukaguzi katika shule ili kubaini
wanafunzi hewa kwenye mpango wa elimu bure.
“Kila mwezi Serikali inapeleka shule
zaidi ya shilingi bilioni 18 kugharamia elimu bure na sasa tumeanza kuona
udanganyifu katika sekta ya elimu kwa kuwa na wanafunzi hewa. Wakuu wa Wilaya
na Maofisa Elimu nendeni mkafanye ukaguzi ili mpate takwimu sahihi,“amesisitiza.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Alhamisi, Agosti
18, 2016) alipokutana na watumishi na viongozi wa Manispaa ya Ilala katika
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Wakuu wa Wilaya na Maofisa Elimu
mkiona takwimu ziwachanganya, ni lazima mtoke maofisini na kwenda katika shule
zilizo kwenye mpango wa elimu bure mkafanye uhakiki wa idadi ya wanafunzi,” alionya.
Wakati huo huo Waziri
Mkuu amesema maamuzi yanayotolewa kwenye vikao vya madiwani lazima yawe
na tija na ameitaka halmashauri hiyo kuhakikisha fedha zinazokusanywa
zinatumika kuboresha shunghuli za maendeleo badala ya kujilipa posho.
“Lazima mjipange vizuri na kupunguza
changamoto zinazoikabili wilaya yenu. Malipo yote ni lazima yawe yale
yaliyoainishwa katika waraka na si vinginevyo.Mtu wa Ilala unadai nauli ya sh.
200,000; hivi unakuwa unatoka wapi hata mimi wa Lindi silipwi nauli hiyo,” alihoji.
Waziri Mkuu alisema ni lazima halmashauri zote
nchini zizingatie sheria za Mamlaka ya Serikali za Mitaa na watendaji wake
wajiulize kama mambo wanayoyafanya yana tija na wanawatendea haki watu
wanaowatumikia.
Alisema Serikali inataka kuwa na watumishi
wanaotambua nafasi zao na watakaofanya kazi kwa uadilifu, uaminifu pamoja na
uwajibikaji mkubwa hivyo kila mtu ahakikishe anafanya kazi vizuri na yenye
matokeo chanya.
“Kuna watu wanaona ukuu wa idara ndiyo
kila kitu, hata yule anayekimbiza mafaili hathaminiwi, hili si jambo jema!
Ninyi wote ni kitu kimoja, ni watumishi wa Serikali, hivyo kila mmoja amthamini
mwenzake,” alisema.
Waziri Mkuu alisema: “Mkurugenzi yeyote
asikubali kuwa na wakuu wa Idara wasiokuwa na ushirikiano na watumishi wengine
kwa sababu hataweza kupata mafanikio ya kiutendaji ndani ya eneo lake,”.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
ALHAMISI, AGOSTI 18, 2016.