UKAWA WAMWANDAMA RAIS MAGUFULI,WAIBUKA NA HILI,SOMA HAPO KUJUA
![]() |
John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania |
RAIS John
Magufuli anaandamwa, sasa anatakiwa kuwachukulia hatua wakurugenzi, watendaji
na makatibu tawala wa mikoa waliosababisha kuwepo kwa watumishi hewa, anaandika Aisha Amran.
Wabunge na viongozi wa vyama vinavyounda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wamekuwa wakimtaka Rais Magufuli kuchukua hatua
dhidi ya wale wanaofuja fedha za umma.
Safari hii Ruth Mollel, Waziri Kivuli na Msemaji Mkuu wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni-Ofisi ya Rais (Utumishi) amesema, endapo Rais
Magufuli atashindwa kuwachukulia hatua watumishi hao, atakuwa hajatimiza wajibu
wake.
Amesema, sababu inayochangia kuwepo kwa watumishi hewa ni
udhaifu wa Tume ya Utumishi wa Umma kutohakiki mfumo wa rasilimali watu pia
kukoseka kwa vitendea kazi ili watekeleze jukumu la kuhakiki watumishi wa umma
na kisha kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Amesema “watumishi hewa ni tatizo la kutengenezwa kwa makusudi
kwani mabilioni yanayopotea kila mwaka kutokana na malipo ya watumishi hewa
yanakwenda kwenye mifuko binafsi ya viongozi na watendaji.”
Amesema, licha ya kelele na jitihada zote na taarifa rasmi za
kila mwaka za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesaba za Serikali (CAG) kuonesha
ukubwa na upana wa tatizo, hakuna kiongozi wala mtendaji wa idara ya serikali
au taasisi ambaye amewajibishwa.
“Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za Serikali za Mitaa ndio
waajiri wa watumishi katika halmashauri zao. Kwa sababu hiyo, Wakuu wa Mikoa na
Wakurugenzi wa Halmashauri wanahusika moja kwa moja na uwepo wa watumishi hewa
katika mikoa na katika halmashauri za serikali za mitaa.
“Hawa ndio ambao wamepewa jukumu na Rais Magufuli la kuwabaini
watumishi hewa katika maeneo yao na kutoa taarifa,” amesema Mollel na kuongeza;
“Tunasubiri kuona hatua zitakazochukulia na Rais Magufuli dhidi
ya wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri ambao kwa makusudi au kwa
uzembe wao wamesababisha kuwepo kwa watumishi hewa katika mikoa na halmashauri
zao.”
Hakuna maoni
Chapisha Maoni