Zinazobamba

RAIS MAGUFULI ASIUMBE MANENO KWA MOYO,SOMA HAPO KUJUA



 John Magufuli, Rais wa Tanzania

NINA orodha ndefu ya kauli za Rais John Magufuli, hasa zilizo tata. Zile zinazozua mjadala katika jamii, anaandika Ansbert Ngurumo.

Kama alivyokiri mwenyewe wiki kadhaa zilizopita mbele ya viongozi wenzake wa Afrika Mashariki, jijini Arusha, Rais Magufuli anazungumza kutoka moyoni, siyo kutoka kichwani.

Tatizo la kutoa kauli moyoni ni kuzungumza kwa hisia na kupoteza umakini utokanao na fikra pevu na tafakuri izaayo busara kabla ya mzungumzaji kusema.

Matokeo ya kutoa kauli ya moyoni, inapoleta tatizo, mzungumzaji akahojiwa, hukumbilia kuikana – ama kwa kujitenga na athari mbaya za kauli yenyewe, au kwa kutokumbuka kwamba iliwahi kutolewa, kwa sababu haikutoka akilini, bali moyoni.

Moyo haukumbuki. Kazi ya moyo ni kuhisi. Moyo hupenda na huchukia. Waingereza husema, “follow your heart but take your brain with you.” Kwa Kiswahili chepesi, tunaweza kuutafsiri hivi: “Fuata utashi wako, lakini chukua tahadhari.”

Wakati mwingine, viongozi wetu hawachukui tahadhari kabla ya kusema yaliyo mioyoni mwao. Wanaweza kuwa na nia njema, wakaiharibu kwa jinsi wanavyofikisha ujumbe wao kwa umma.

Labda John Lennon, mwimbaji na mtunzi wa nyimbo mashuhuri (1940-1980), alikuwa sahihi aliposema, “unapokuwa unazama, huwezi kufikiri.”

Bado natafakari kauli ya Rais Magufuli mwanzoni mwa Januari 2012, akiwa Waziri wa Ujenzi, alipowataka wakazi wa Kigamboni na Dar es Salaam wakubaliane na ongezeko la asimilia 100 ya nauli ya kivuko, kati ya Magogoni na Kigamboni, na akasisitiza kuwa asiyeweza kulipa nauli, apige mbizi.

Alikuwa analazimisha wananchi wakubaliane na pendekezo la wizara yake kupandisha nauli ya kivuko kutoka Tsh 100 hadi 200.
Alisema: “Asiyetaka kulipa nauli hiyo, apige mbizi baharini na kama hawezi azunguke Kongowe, kuingia katikati ya jiji au arudi kijijini akalime.”

Kauli yake ilikera wananchi wengi, wakiwamo waandishi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa, kiuchumi na kisiasa.
Miongoni mwa waliokosoa kauli ya Magufuli ni Maggid Mjengwa, mwandishi na mchambuzi aliyemtaka Magufuli aombe radhi wakazi wa Kigamboni.

Aliita kauli hiyo kuwa ni “mchemsho wa kwanza wa mwaka.” Alitaka Watanzania wampime Magufuli kama anastahili kukaa tena katika wizara hiyo.

Alisisitiza: “Magufuli huenda amekaa muda mrefu serikalini, kiasi cha kupoteza mguso na hali halisi za Watanzania. Kauli aliyotumia ni kielelezo cha kupoteza mguso huo na hali halisi inayowakabili Watanzania walio wengi, miongoni mwao ni wakazi wa Kigamboni.”

Kuna watu walifananisha kauli hiyo na ile iliyowahi kutolewa na Basil Mramba, alipokuwa waziri wa fedha katoka serikali ya awamu ya tatu, kwamba – “hata ikilazimu wananchi kula nyasi, watakula tu, ili ndege ya rais inunuliwe.”

Agosti 2015, alipokuwa ameteuliwa kuwa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Magufuli alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa akishapata urais atanunulia walimu wote laptopu.

Katika safu yangu ya Maswali Magumu, katika gazeti la Tanzania Daima, nilihoji umakini wake, nikaonesha kasoro ya kauli hiyo, nikaorodhesha matatizo lukuki ya walimu na mfumo wa elimu nchini. Nilihoji kwanini yeye anaona laptopu ndicho kipaumbele cha elimu na walimu.

Magufuli aliposoma uchambuzi wangu, hakuupenda. Lakini alikuwa na ujasiri wa kutosha kufuatilia mwenyewe na kuonesha hisia zake. Akanipigia simu, akazungumza kwa upole na utaratibu. Sijawahi – kabla na baada ya simu hiyo – kusikia Magufuli akiwa mpole kiasi kile.

Alisisitiza kuwa hajawahi kusema popote kuwa atawapatia walimu laptopu. Alidai kwamba alinukuliwa kisiasa. Alisema inawezekana amelishwa maneno kwa sababu anagombea urais.
Kabla hajakata simu, alinieleza pia kuwa haikuwa mara yake ya kwanza kulishwa maneno. Akasema kuwa hata ile kauli ya kupiga mbizi ilipikwa. Alisisitiza kuwa hajawahi kutoa kauli hiyo.
“Walinisingizia. Sikuwahi kusema kwamba watu wapige mbizi.” Nilimweleza kwa upole, “nimekusikia mheshimiwa.”
Kwa sababu hiyo, Rais Magufuli hakuwahi kuomba radhi wananchi wa Kigamboni, kwa kuwa anasisitiza kwamba hajawahi kutamka maneno hayo. Ushauri wa Maggid ulipotea bure!
Nikamsikia tena siku ya kuadhimisha Wiki ya Sheria, miezi mitatu baada ya kuwa rais. Alimweleza Chande Othman, Jaji Mkuu, kwamba ana taarifa kuwa kuna mahakimu wametoa hukumu 900 kwa mwaka, na akaagiza kwamba ni lazima mahakimu wa mahakama za mwanzo watoe walau hukumu 260 kwa mwaka; akasema, wasipofikisha idadi hiyo, nao watakuwa majipu ambayo lazima Jaji Mkuu ayatumbue. Waliomsikiliza wakapiga makofi!
Akaongeza: “…Jaji Mkuu, unatoa maagizo hakimu atoe hukumu angalau kesi 260, halafu mtu huyohuyo anapinga agizo lako, na bado unamwangalia tu, halafu leo unasema unampa siku saba…. Ninachotaka kukuomba, wale waliohukumu kesi 900, nami nawapongeza….”
Baadaye tulisikia miong’ono kutoka kwa wajuzi wa masuala ya sheria na utoaji haki, wakisema rais alidanganywa. Mwaka mmoja una siku 365. Katika mwaka hakimu ana siku 28 za likizo.
Ili hakimu aweze kufikisha hukumu 900 kwa mwaka, lazima awe anaandika hukumu zaidi ya mbili kila siku. Ataweza kuhukumu kesi kila siku? Haiwezekani!
Akasema, “msifikiri mimi ni mnyama sana. Mimi ni mpole sana….”
Wengine tukashtuka. Nani ataamini kwamba Magufuli ni mpole sana? Na nani alimwambia kuwa yeye ni “mnyama sana au kidogo?” Haya ni maneno yatokayo moyoni.
Ikaja Februari 6, katika maadhimisho ya miaka 39 ya CCM, mkoani Iringa, akasema: “…Na nitoe wito kwa watendaji wote wa serikali, kuanzia juu mpaka chini, anayejijua ni mtendaji wa serikali, ana jukumu moja tu la kutekeleza ilani ya CCM. Mimi ni rais, lakini ni rais niliyechaguliwa na CCM…hakuna mtawala yeyote anayependa kutawaliwa, na bahati mbaya atawaliwe na vyama vya hovyohovyo…”
Nikamsikia tena Machi 15, mwaka huu, akiwaambia wakuu wapya wa mikoa, “…mna mamlaka ya kuwaweka ndani hata masaa 48; wekeni ndani mpaka wapate adabu.”
Juzijuzi akiwa nyumbani kwao Chato, mkoani Geita, alisema, “kuna watu wana mishahara mikubwa wanaishi kama malaika; na kwamba anataka aishushe ili waishi kama shetani.”
Nikashtuka na kuhoji, “Rais anataka kuongoza mashetani?” Nina shaka kama akiulizwa leo atakumbuka kauli hiyo au atasema amelishwa maneno.
Ninapochanganya kauli zote hizi, naanza kuelewa kwanini aliniambia kuwa hajawahi kutamka maneno ya kupiga mbizi na kununua laptopu. Alishasahau kwa sababu aliyasema kutoka moyoni. Hakuyatoa kichwani.
Ushauri wangu ni huu. Rais Magufuli ajenge utaratibu wa kuchukua tahadhari anapozungumza na wananchi. Wahenga walisema “maneno huumba.” Na Biblia inasema, Mungu aliumba kwa neno lake. Magufuli naye aumbe kwa neno litokalo kichwani, siyo moyoni.
Makala hii imechapishwa kwenye Gazeti la MwanaHALISI toleo la 334 la tarehe 11-17 Aprili mwaka huu.

Hakuna maoni