BILIONEA LUGUMI AICHANGANYA SERIKALI YA MAGUFULI,KAMPUNI YAKE NI PASUKA KICHWA,WASOMI WAHOJI ILIPOISHIA KASI YA UTUMBUAJI MAJIPU,SOMA HAPO KUJU
SAKATA la ufisadi kuhusu mkataba kati ya Kampuni ya
Lugumi Enterprises Ltd na Jeshi la Polisi nchini sasa limechukua sura mpya huku
moja ya kampuni kubwa ya Marekani ikitajwa.
Hatua hiyo imekuja huku kukiwa na utata kuhusu
mkataba huo ambapo sasa Kampuni ya Biometrica LLC ya Marekani ikihusishwa na
sakata hilo.
Inaelezwa mwaka 2011, Kampuni hiyo ya Kimarekani
iliwasilishwa na Kampuni ya Teknolojia ya Infosys IPS Tanzania Limited, ambapo
waliingia nayo mkataba wa kufunga baadhi ya mashine hizo za kuchukua alama za
vidole katika vituo vya polisi nchini.
Baada ya kukamilika kwa kazi hiyo bado haijatajwa ni
vituo vingapi Infosys Tanzania Limited ilifunga mashine hiyo.
Akizungumzia mkataba huo, Naibu Meneja Mkuu wa
Infosys, Sweki Donald, alisema wakati wote wakiwa wanaendelea na kazi
hawajawahi kushirikiana na Kampuni ya Lugumi Enterprises.
“Mwaka 2011 tulipata kazi ya kufunga mashine za
kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi na kazi hii sisi tuliipata
kupitia Kampuni ya Biometrica LLC ya nchini Marekani ambao wao walisema
wamepata taarifa zetu kupitia Kampuni ya Dell ya Marekani.
“Tulifanyakazi yetu kwa mujibu wa mkataba na baada
ya kumaliza tulilipwa Dola 74, 420 (sawa na shilingi 162,849,565), ila
ninapenda kusema kuwa wakati wote hatukujua kama kuna mtu anaitwa Lugumi.
“Tumekuja kujua baadaye sana hivyo ninapenda kusema
hapa kuwa hatuhusiki na Lugumi na wala hatumjui,” alisema Sweki wakati wa
mahojiano na mwandishi aliyejitambulisha wa Focus Media.
Naibu Meneja huyo alipoulizwa kuhusu ushiriki wa
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, alisema waziri huyo alikuwa
ni mmoja wa waasisi wa kampuni hiyo ingawa aliondoka tangu mwaka 2010.
“Charles Kitwanga ni mmoja wa founder wa Infosys
Tanzania Limited, tangu mwaka 2010 aliondoka katika kampuni na amekuwa hana
mawasiliano,” alisema Sweki.
Alisema wao kama Infosys Tanzania Limited,
hawahusiki na kashfa ya ufisadi huo unaoripotiwa sasa.
Katika kile kinachoonekana ni filamu hasa baada ya
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kutoa siku tatu kwa kampuni hiyo
kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa mradi wa kufunga mashine za utambuzi wa
alama za vidole katika vituo 108 nchini, sakata hilo limekuwa likichukua sura
mpya kila kukicha.
Uamuzi huo uliibua hisia miongoni mwa jamii ambapo
katika kipindi cha siku mbili baada ya PAC kutaka ripoti hiyo, Kamati ya Bunge
ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, iliingilia kati ambapo mwenyekiti wake
Balozi Adadi Rajabu, alikiri kupokea mkataba huo.
Hali hiyo ilizua sintofahamu miongoni mwa wajumbe wa
Kamati za Bunge huku baadhi yao wakihofu hatua hiyo huenda ikawa ni mkakati wa
kuficha ukweli dhidi ya vigogo waliotajwa katika mkataba huo tata wa Sh bilioni
37.
Kauli ya Bunge
Pamoja na jana kuwa ni siku ambayo ilitarajiwa
kampuni hiyo ingewasilisha, hatimaye jana Ofisi ya Bunge kupitia Kitengo cha
Habari, Elimu na Mawasiliano, ilieleza kuwa taarifa hiyo itawasilishwa Aprili
18, mwaka huu.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba tangu lilipoibuliwa
sakata hilo na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Aprili 5, mwaka huu
baada ya Jeshi la Polisi kutakiwa kuwasilisha mkataba ulioingiwa kati ya
Jeshi hilo na Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd kuhusu mradi wa Utambuzi wa
Alama za Vidole AFIS (Automated Fingerprint Identification System), kumekuwa na
taarifa ambazo si sahihi.
“Ukweli kuhusu jambo hili ni kwamba, Aprili 5 mwaka
huu, kamati hiyo ilikutana na kujadili taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu
zilizokaguliwa za fungu 28, Jeshi la Polisi kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni
30, 2014 ambapo kamati pamoja na mambo mengine ilibaini dosari katika
utekelezaji wa mkataba huo.
“Kutokana na dosari hizo, kamati iliomba Ofisa
Masuhuli ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
kuwasilisha maelezo ya kina kwa maandishi kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa
Ofisi ya Katibu wa Bunge ili kamati iweze kuchambua na kujadili maelezo
hayo kabla ya kupendekeza kwa Bunge hatua zaidi za kuchukua.
“Kutokana na agizo hilo, kamati ilimwandikia pia
Katibu wa Bunge taarifa kuhusu agizo hilo Aprili 12 mwaka huu, ili kupatiwa
maelezo hayo kutoka kwa Ofisa Masuhuli. Aidha, Ofisi ya Bunge ilimwandikia
barua Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani Aprili 12 mwaka huu kuwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) iliyotokana na kikao hicho cha Aprili 5 mwaka huu kabla ya
Aprili 18 mwaka huu kama ilivyoshauriwa na kamati,” ilieleza taarifa hiyo.
Sarakasi zaidi
Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd inadaiwa kupewa tenda
na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole
katika vituo 108 nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37.
Hadi sasa mashine hizo zimefungwa katika vituo 14
vya polisi pekee na tayari kampuni hiyo imelipwa Sh bilioni 34 ambazo ni sawa
na asilimia 99 ya fedha za mkataba.
Kamati ya PAC ambayo ilibaini kuwapo viashiria vya
ufisadi katika zabuni, iliwaagiza watendaji wa jeshi hilo kuwasilisha taarifa
za mkataba huo, lakini mkataba huo ulihamishwa na kupelekwa Kamati ya Bunge ya
Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Lugumi ambaye anatajwa kuwa na uhusiano wa kifamilia
na baadhi ya vigogo nchini, aliingia mkataba tata na Jeshi la Polisi mwaka 2011
kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya
polisi, lakini kazi hiyo haikufanyika kwa ufanisi licha ya kulipwa mabilioni ya
fedha.
Chanzo cha kuaminika kililiambia gazeti hili kuwa
mfanyabiashara huyo amekwenda nje kununua mashine zilizosalia kama njia ya
kuzima mjadala kuhusu utata wa mkataba huo ambao unaelezwa kumhusisha kigogo
mmoja katika Serikali ya Rais Dk. John Magufuli.
Utata
Katika sakata hilo inadaiwa kuwa Kampuni ya Lugumi
Enterprises ilipewa zabuni ya kufunga mashine za ‘Biometric Access’ kwa ajili
ya kuchukua alama za vidole ikiwa haina uzoefu wa kazi hiyo.
“Wamepewa mkataba sawa, lakini mbona taarifa
zinaonyesha kuwa kampuni hii haijasajiliwa kama Biometric Access Company na
haijawahi kufanya kazi zozote zinazohusiana na Biometric Access Control?”
alihoji mmoja wa wataalamu ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni