Zinazobamba

TAARIFA MUHIMU KUHUSU AFYA YA ASKOFU MWADHAMA POLYCARP KARDINALI PENGO,SOMA HAPO KUJUA



Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amesema afya ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo imeimarika na leo ataruhusiwa.

Kardinali Pengo alifikishwa katika hospitali hiyo Desemba 31, mwaka jana kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

Profesa Janabi alisema Pengo alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo. Hata hivyo, hakueleza kwa undani.

Jana, kwa mara ya kwanza tangu afikishwe katika hospitali hiyo, Pengo alijitokeza hadharani na kuzungumza na wafanyakazi wa taasisi hiyo na waandishi wa habari, huku akishukuru kwa huduma alizopata.

Alisema amepatiwa huduma nzuri na kumfanya afute kichwani mwake habari za watu mbalimbali wanaodai kuwa MNH haiwahudumii vizuri wagonjwa.

“Nataka niwashukuru wahudumu wote walionifikisha katika hali hii, hasa Profesa Janabi na Mkuu wa Kitengo cha Dharura na Ajali, Dk Juma Mfinanga,” alisema.

Akiwa hospitalini hapo jana, Kardinali Pengo alitembelewa na maaskofu wasaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Titus Mdoe na Eusebius Nzigilwa pamoja na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea, Damian Dallu.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu alisema Serikali imejipanga kuhakikisha wagonjwa wa moyo hawapelekwi nje ya nchi kutibiwa.

Alisema tangu kuanza kwa mpango wa kuwatibu wagonjwa hao nchini Taifa limeokoa takribani Sh5 bilioni.

“Tutatoa vibali kwa wagonjwa kutibiwa nje ya nchi ikiwa itathibitishwa na madaktari kuwa huduma husika haiwezi kutolewa nchini,” alisema.

 Jana, Profesa Janabi alisema waliwahudumia wagonjwa 500 na mwaka huu wanatarajia kupokea kundi la madaktari bingwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kutoa mafunzo.     

Mpekuzi blog

Hakuna maoni