POLISI WAUANA WENYEWE KWA WENYEWE KISA MAPENZI,SOMA HAPO KUJUA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus
Kamugisha
Polisi Mwanza amuua mwenzake na kujiua
HALI isiyokuwa ya
kawaida, askari Polisi wawili wamefariki dunia katika Wilaya ya Nyamagana
jijini Mwanza, baada ya mmoja wapo kumpiga risasi mwenzake kisha na yeye
kujipiga risasi. Anaandika Moses Mseti, Mwanza …
(endelea).
Tukio hilo limetokea leo saa 8:30 mchana
katika eneo la benki ya Posta iliyopo barabara ya Nyeyere, baada ya askari
polisi aliyekuwa amevalia kiraia kufika kwenye benki hiyo kupata huduma ambapo
ndipo tukio hilo likatokea.
Pia inadaiwa kuwa
polisi hao walifikia hatua hiyo baada ya kudaiwa kuwepo kwa ugomvi wa muda
mrefu ambao unadaiwa unatokana na wivu wa kimapenzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Mwanza, Justus Kamugisha, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo
amesema kuwa marehemu aliyejiuwa hakuwa na tatizo lolote la kiafya na wala
wakati wote hakuonekana kuwa na msongo wa mawazo.
Kamugisha alimtaja
askari aliyempiga risasi mwenzie kisha na yeye kujiua kuwa ni namba H. 852 PC
Masunga Elisha, ambaye alikuwa na mwenzake namba H. 4291 PC Remigius Alphostin
kwenye lindo la benki ya Posta jijini Mwanza.
Pia Kamugisha alimtaja
marehemu aliyepigwa risasi kuwa ni namba H. 5950 PC Petro Matiko, ambaye
alifika katika eneo hilo la benki kupata huduma ambapo ndipo tukio hilo la
kusikutisha kutokea.
“PC Matiko (marehemu
Petro Matiko) alifika katika eneo la benki kupata huduma za kibenki lakini baada
ya kutoka ndani alisalimiana na wenzake na kuwaeleza kwamba mtandao
unasumbua, huku akimuuliza kwanini unaikoki silaha unafahamu kama ni hatari
lakini PC Masunga alimwambia aachane nae ndipo akampiga risasi,” amesema
Kamugisha.
Hata hivyo baada ya PC
Masunga kutekeleza tukio hilo pia na yeye alijipiga risasi katika eneo la
kidevu karibu na mdomoni na kupoteza maisha papo hapo.
Kamanda Kamugisha
amesema kuwa mpaka sasa chanzo cha tukio la askari hao kufanya tukio hilo
hakijafahamika na kwamba wanaendelea na uchanguzi wa tuki hilo.
Mashuhuda.
Baadhi ya mashuhuda wa
tukio hilo, Marwa Ezekiel na Neema Daud, wamesema kuwa baada ya kusikia mlio wa
risasi baadhi ya wateja waliokuwa katika benki hiyo walianza kufunga mlango wa
kuingia benki.
Pia wamesema kuwa baada ya dakika tano kupita walisikia mlio mwingine wa risasi
wakati walipotoka nje walimuona askari aliyejiua akiwa amelala karibu na mlango
huo wa kuingia katika benki hiyo.
“Sisi tulikuwa ndani
ya benki lakini wakati tukiendelea na huduma ghafla tulisikia mlio lakini baada
ya dakika tano tukasikia mlio mwingine ndipo watu wakaingia ndani,” amesema
Neema Daud.
Hata hivyo amesema kuwa wakati mlio wa risasi ya kwanza unasikika walizani ni
mlio wa pikipiki lakini baada ya kusikia mlio wa pili ndipo wakatoa nje na
kuona marehemu hao wakiwa wamelala chini.
Watu wa karibu na
marehemu
Hata hivyo baadhi ya
watu wa karibu na marehemu hao, ambao hawakutaka majina yao kuandikwa kwenye
gazeti walisema kuwa marehemu hao walikuwa na ugomvi wa muda mrefu huku wengine
wakilihusisha tukio hilo na masuala ya kuzulumiana fedha.
“Hawa jamaa (marehemu
wawili) hawawezi kufanyiana tukio la namna hii, ukiangalia kwanza yule
aliyepigwa risasi (Petro Matiko) wakati alipoingia ndani hakuwaongelesha lakini
alipotoka ndipo akawaeleza mtandao unasumbua hapo lazima kuna kitu,” amesema
mtu ambaye hakutaka kutajwa kuandikwa jina lake.
Hata hivyo alidai
kwamba awali walikuwa wakisikia kwamba marehemu hao wanadaiana fedha hivyo
hawakufahamu ni kiasi gani na walikopeshana namna gani.
Tukio hilo la Polisi
kuua mwenzake na kisha yeye kujiua limegusa hisia tofauti kwa wakazi wa
Jiji la Mwanza, ambapo watu waliozungumza na gazeti hili wasema kuwa tukio hilo
ni la mara ya kwanza kutokea katika mkoa huo.
Abdalah Hussein na
Elisha Hezron ni wakazi wa jijini hapa wamesema kuwa tukio lazima jeshi la
Polisi kufanya uchunguzi wa kina kwani askari aliyepitia mafunzo hawezi kufanya
tukio la namna hiyo.
“Kwanza ni kitu ambacho hakiingii kichwani kwangu na hata kwa watu wengine hivi
askari aliyepitia mafunzo kupiga risasi mbele ya watu tena benki, uchunguzi
unapaswa kufanyika wa kina,” amesema Hussein.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni