MANJI WA YANGA AONYWA,,SOMA HAPO KUJUA
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki amemuomba
mmiliki wa Kampuni ya Q Consult inayomilikiwa na mfanyabiashara Yussuf Manji
kutumia busara kukubali kuuachia ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Sadiki alisema Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi katika uamuzi wake
imeiamuru Manispaa ya Kinondoni, kutekeleza mkataba wake na kampuni ya Q
Consult kwa ajili ya kampuni hiyo kuendeleza ufukwe huo hata hivyo Manispaa ya
Kinondoni imekata rufaa.
“Kampuni ya Q Consult kwa busara tu iachane na kesi, ikubali
kurudisha ufukwe huo chini ya mamlaka ya Kinondoni ili iweze kuuendeleza ufukwe
huo kwa manufaa ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam na sio kwa manufaa ya mtu
mmoja kama anavyotaka mtu huyo,” alisema Sadiki.
Alisema wananchi wafahamu kuwa ufukwe huo wa Coco haujauzwa,
kama watu wanavyodai na kwamba kesi hiyo iko mahakamani, ambapo Ofisi ya
Manispaa ya Kinondoni kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamekata rufaa.
Akielezea sakata hilo, Sadiki alisema kampuni ya Q Consult
inayomilikiwa na Manji mwaka 2007 iliingia mkataba na Manispaa ya Kinondoni
kuendeleza ufukwe huo.
Alisema, hata hivyo, baadaye Manispaa ya hiyo ilivunja mkataba
huo baada ya Kampuni ya Q Consult kushindwa kutimiza masharti, jambo ambalo
liliifanya kampuni hiyo kwenda mahakamani.
Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi iliamuru Manispaa ya
Kinondoni, kutekeleza mkataba wake na kampuni hiyo kwa ajili ya kuendeleza
ufukwe huo.
“Kama nilivyosema kupitia mwanasheria mkuu wa Serikali tumekata
rufaa katika uamuzi huo kwasababu tunaamini haukuwa sahihi, hata hivyo
mwekezaji huyo namshauri tu anaweza kufanya maamuzi akaachana na kesi hiyo na
kuamua kurudisha ufukwe huo uendelee kutumiwa na Watanzania wote,” alisema Sadiki.
Kwa kampuni hiyo kushinda kesi hiyo, inamaanisha kuwa mwekezaji
huyo endapo ataendeleza eneo hilo, wananchi hawatakuwa na fursa hiyo tena, kama
wanavyoutumia sasa.
Sadiki alisema tayari serikali imefanya mazungumzo na moja na
benki hapa nchini kwa ajili ya kupata mkopo, ambao utasaidia kuendeleza eneo
hilo ili liendelee kubaki chini ya Manispaa ya Kinondoni na kutumiwa na watu
wote
Hakuna maoni
Chapisha Maoni