LOWASSA KUIBUKIA KWENYE UBUNGE WA LEMA ARUSHA,SOMA HAPO KUJUA
Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Edward Lowassa, anatarajiwa kuanza kambi nzito jijini Arusha kuanzia
keshokutwa (Jumatano) kwa nia ya kuhakikisha kuwa mgombea ubunge wa chama chake
katika katika Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema anatetea kiti chake kwa
ushindi wa kishindo.
Taarifa ambazo Nipashe ilithibitishiwa
jana na watu wa karibu wa Lowassa zilieleza kuwa
(Lowassa) ataungana na timu ya kampeni ya Chadema kujichimbia jijini Arusha kwa
siku zote zilizobaki za kampeni kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo Jumapili
ijayo.
Uchaguzi wa kumpata Mbunge wa Arusha Mjini haukufanyika Oktoba
25, 2015 kama ilivyokuwa kwa majimbo mengine nchini kufuatia kifo cha mgombea
wa ACT-Wazalendo, Estomiah Mallah.
“Ni kweli, Lowassa atapiga kambi Arusha kuanzia Jumatano
(keshokutwa) kwa ajili ya kuungana na kina Lema ili kuhakikisha kuwa jimbo hilo
linarejea mikononi mwa Chadema kwa ushindi wa kishindo, “ chanzo kiliiambia
Nipashe jana.
Kadhalika, ilielezwa kuwa hatua hiyo ya Lowassa ni muendelezo wa
ushiriki wake katika kuiimarisha Chadema kwa nia ya kuleta ukombozi wa kweli
kwa Watanzania. Hivi karibuni alikuwa Mwanza na Geita kwa siku kadhaa katika
kushughulikia mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Geita,
Alphonce Mawazo, ambaye aliuawa kinyama na watu wasiojulikana.
LEMA MATUMAINI 100%
Katika hatua nyingine, Lema anayegombea kutetea jimbo hilo,
alisema ushindi kwake na chama chake uko wazi kwani wananchi wameamka na wengi
wamepania kumrejesha madarakani.
Alisema kampeni zake za nyumba kwa nyumba ndizo zinazomuongezea
uhakika wa kushinda kwani hupokewa vizuri na wote humuahidi kujitokeza kwa
wingi Jumapili ili kumchagua.
“Kwa kweli sijaona nitashindwaje kurudisha ubunge wangu,
wananchi wangu wananipa moyo sana,” alisema.
Akizungumza katika mkutano wake wa kampeni jana, Lema alisema
atakapochaguliwa, kazi kubwa atakayoifanya ni kuhakikisha kuwa mapato ya Halmashauri
ya Jiji yanaongezeka ili kufanikisha dhamira ya kuboresha huduma za jamii kwa
wananchi
Hakuna maoni
Chapisha Maoni