BAADA YA MAGUFULI KUNYIMWA RASMI MISAADA NA MAREKANI ,FREEMAN MBOWE AIBUKA NA KUMLIMA TAMKO KALI,SOMA HAPO KUJUA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KAULI YA MWENYEKITI FREEMAN MBOWE
KUHUSU
UAMUZI WA BODI YA MCC KUZUIA MSAADA WAKE KWA
SERIKALI YA TANZANIA
Muda mfupi baada ya Bodi ya MCC kutoa taarifa
inayoonesha Tanzania haitapata msaada kutoka shirika hilo kama ilivyotarajiwa
kwa ajili ya mwaka 2016, Mwenyekiti wa Chama (T), Freema Mbowe ametoa kauli
nzito juu ya suala hilo akisema kuwa kuchelewa kupatikana kwa fedha za MCC si
tu kunachafua jina la nchi na hadhi yake katika medani za kimataifa, bali kutaathiri
kwa kiasi kikubwa miradi yote iliyo chini ya ufadhili wa MCC.
MCC imeahirisha msada huo wa USD Mil. 472.8 ambazo
ni takriban trilioni moja kwa fedha za Tanzania zilizolengwa kusaidia sekta ya
nishati ya umeme hususan ule wa vijijini, katika kuunganisha wateja wapya,
mabadiliko ya kimuundo ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) ili lifanye kazi na
kutoa huduma kwa ufanisi katika sehemu za uzalishaji, usafirishaji na
usambazaji.
Fedha hizo pia zilikusudiwa kusaidia kuanza kwa
mpango mkubwa wa kuboresha sekta ya umeme nchini.2014-2024.
Mbowe amemtaka Rais John Magufuli kuchukua hatua za
haraka za kiuongozi kumaliza mtanziko wa kisiasa Zanzibar kwa mshindi wa nafasi
ya urais kutangazwa kutokana na uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba, mwaka huu.
Aidha amesema kuwa Sheria ya makosa ya mtandao
(Cyber Crime Act 2015) ambayo ni mojawapo ya sababu zilizotumiwa na MCC
kuahirisha msaada huo kwa Tanzania hadi itakapokuwa imefanyiwa kazi, ni sheria
mbaya sana inayokinzana na kukua kwa technologia ya habari na mawasiliano na
kuzuia upashanaji wa habari miongoni mwa jamii ambayo ililenga kuweka makosa ya
kijinai ili kudhibiti wapinzani wa CCM katika uchaguzi mkuu na kukipatia
mazingira ya ushindi chama hicho.
"Sasa imethibitika kuwa Bodi ya MCC iliyokaa
tarehe 16 Dec 2015 imeahirisha rasmi kuidhinisha msaada wa Millenium Challenge
uliokuwa umekusudiwa kwa Tanzania kwa mwaka wa fedha 2016. Sababu kuu mbili
zilizosababisha uamuzi huo ni:
1. Mkwamo wa Uchaguzi wa Rais na Wawakilishi
Zanzibar na
2.Matumizi mabaya ya she ria ya makosa ya mtandao
hususan kuhusiana na uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa
2015."
"Ubabe wa baadhi ya viongozi wa CCM ni janga la
Taifa. Kuchelewa kupatikana kwa fedha za MCC si tu kunachafua jina la nchi na
hadhi yake katika medani za kimataifa, bali kutaathiri kwa kiasi kikubwa miradi
yote iliyo chini ya ufadhili wa MCC," amesema Mwenyekiti Mbowe na
kuongeza;
"Sheria ya makosa ya mtandao (Cyber Crime Act
2015) ni sheria mbaya sana inayokinzana na kukua kwa technologia ya habari na
mawasiliano. Aidha, kwa makusudi kabisa inafifisha uhuru wa kupashana habari na
ni dhahiri ilitungwa kwa nia mbaya ya kuthibiti kijinai uchaguzi mkuu."
"Tuliipinga sheria hii Bungeni na ikapitishwa
usiku wa manane kwa ubabe wa wabunge wa CCM na hata tulipomtaka rais Kikwete
asiisaini aliisaini kibabe akijua anaandaa mazingira gani ya
"kihalifu", " amesema Mwenyekiti Mbowe.
Ameongeza kusema kuwa sheria hiyo ilitumika kuvamia
vituo vya CHADEMA vilivyokuwa vikitumika kukusanya matokeo ya kura za rais na
wabunge na hadi leo vijana zaidi ya 161, wakiwemo wanafunzi, wana kesi za
"kubumba" mahakamani.
Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa Sheria hiyo hiyo
ilitumika kuficha dhana ovu iliyotumika kuhalalisha kuvamia Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC) kilichokuwa kikiratibu watazamaji wa uchaguzi wa ndani
kwa kibali cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
"Vile vile Sheria hii imetumika kuwakamata na
kuwaweka ndani na hata kuwanyima dhamana vijana wetu ambao walituunga mkono
katika uchaguzi mkuu."
"Namtaka rais Magufuli achukue hatua za
kiuongozi na kiutawala kwa kufanya yafuatayo:"
"Kwanza aumalize mgogoro wa kisiasa Zanzibar kwa kuhakikisha
kuwa mshindi halali anatangazwa.
"Pili achukue hatua ya kuifanyia marekebisho
makubwa Sheria ya makosa ya mtandao katika bunge lijalo. Aidha wale wote
waliobambikiwa kesi amuamuru DPP kuzifuta kesi hizo mara moja," amesema.
Mwenyekiti Mbowe amesisitiza kuwa Rais Magufuli hana
budi kuchukua hatua hizo za haraka ili kulinusuru taifa na hasara ya kupoteza
mabilioni hayo ya MCC na zaidi kuepusha kuporomoka zaidi kwa biashara ya utalii
nchini Zanzibar.
Amesema katika taifa ambalo sekta ya umeme
inakabiliwa na matatizo makubwa katika uzalishaji, usambazaji na usafirishaji
huku wananchi wa kipato cha chini wakibebeshwa mzigo mkubwa wa kumudu nishati
hiyo na wengine wakilazimika kutumia nishati mbadala kama mkaa unaotokana na
miti hivyo kusababisha uharibifu wa mazingira, serikali inayojua wajibu wake
yenye viongozi wanaothamini uwajibikaji, haikupaswa kushindwa kuchukua hatua
stahiki kutimiza vigezo vya msaada huo ambao umeshaisaidia Tanzania katika
miradi mingine kadhaa.
Imetolewa leo Ijumaa, Desemba 18, 2015 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
Hakuna maoni
Chapisha Maoni