WANAFUNZI WA CHUO KIKUU WAANZA KUISOMA NAMBA SASA,NUSU YAO WAKOSA MKOPO,SOMA HAPO KUJUA

ZAIDI ya
wanafunzi 50,000 watashindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu kutokana na
kushindwa kupata mikopo kutoka katika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB). Anaandika Charles William … (endelea).
Hayo
yamebainika ikiwa ni siku tatu tangu HESLB kutoa majina ya wanafunzi
waliofanikiwa kupata mikopo kwa mwaka wa masomo 2015/2016, huku idadi kubwa
ikiwa haimo katika majina hayo.
Katika mwaka huu
wa masomo bodi ya mikopo imeweza kuwapatia mikopo wanafunzi 12,000 pekee sawa
na 17.1% ya waombaji zaidi ya 70,000, hivyo kufanya idadi ya wanafunzi
waliokosa mikopo kufikia asilimia 82.9 ya waombaji wote.
Wanafunzi
waliokosa mikopo ya kuwawezesha kujiunga na elimu ya juu na hivyo wazazi wao
kutakiwa kugharamia elimu hiyo wameelezea kusikitishwa na hali hiyo huku
wakiitaka serikali kuwaangalia kwa jicho la kipekee kwani hawana uwezo wa
kuanza masomo pasipo kufadhiriwa na serikali.
Wanafunzi hao
walionekana kukata tamaa ya kutimiza ndoto yao ya kujiunga na elimu ya chuo
kikuu, wamefika makao makuu ya bodi hiyo huku wakiongozana na baadhi ya
viongozi wa serikali ya wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
kutaka kujua hatima yao.
“Nimetokea Tabora, wazazi wangu walinipa Sh. 100,000 ya kutumia
wakiamini tunapewa mikopo na serikali, lakini tumenyimwa na hatujui hatima
yetu, nimebakiwa na Sh. 6,000, naomba serikali ituhurumie, isikie kilio chetu
hatustahili kuteseka hivi,” ameeleza Abdul Omary mwanafunzi mteule UDSM.
Fatuma Bakari, mwanafunzi mwingine kutoka UDSM, amesema: “Siwezi
kujiunga na Chuo bila mkopo, tumefika hapa ili kuomba bodi ya mikopo itusaidie
hatuna tumaini lolote zaidi ya kuomba Mungu atusaidie tuweze kupata mikopo na kuanza
masomo.”
Waziri wa Mikopo serikali ya wanafunzi (Daruso), Shitindi
Venance ameeleza kutokukubaliana na majibu waliyopewa na uongozi wa juu wa bodi
ya mikopo kwani yanakatisha tamaa na kuzima ndoto za wanafunzi wa masikini
kusoma chuo kikuu.
“Hapa UDSM ni wanafunzi 600 tu waliopata mikopo kati ya
wanafunzi 7,000 waliopangiwa kuanza masomo, hili ni janga kubwa kwa watoto wa
masikini kwani hawawezi kujisajili chuoni wala kupata makazi katika mabweni
mpaka walipe ada na wengi wametoka mikoani.
“Tunachukua hatua moja mbele na kuamua kulifuatilia suala hili
kwa katibu mkuu wa wizara ya elimu na katibu mkuu wa wizara ya fedha kwa sababu
bodi bado wanasisitiza tuwe na subira ilihali muda umeenda na wanafunzi
wanateseka” ameeleza Shitindi.
Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Omega Ngole
amewaambia wanahabari waliofika ofisini kwake kuwa bodi haistahili kulaumiwa
kwani serikali kupitia wizara ya fedha na wizara ya elimu ndio yenye uwezo wa
kutenga kiasi cha fedha kulingana na mahitaji ya wakati husika.
“Lengo la bodi ya mikopo ni kuwawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu
kusoma kwa ufadhili wa serikali na wala sio kuwakwamisha, tunaendelea
kujadiliana na serikali kuona kama itatuongeza fedha ili tuweze kutoa awamu ya
pili ya majina ya wanafunzi waliopata mikopo, tunawaomba wanafunzi wavute
subira,” anaeleza Ngole
Hata hivyo Ngole amesema hawezi kusema lini watatangaza majina
ya awamu ya pili kwani hilo linategemea ni lini serikali itatoa fedha kwa ajili
ya wanafunzi wa awam ya pili.
Katika mwaka uliopita wa masomo 2014/2015 serikali ilitoa mikopo
kwa wanafunzi 30,000 sawa na 51.7% ya waombaji wote 58,000 na hivyo kufanya
waliokosa mikopo kuwa wanafunzi 28,000 sawa na 49% pekee tofauti na mwaka huu
ambapo waliokosa wamefikia asilimia 82.9
1 comment
mungu tutangulie
Post a Comment