MAGUFULI AMKABA KOO BAKHARESA,UTAPELI WAKE BANDARINI WAMWEKA MSALABANI,SOMA HAPO KUJUA
*TRA yazuia makontena yake bandari kavu
*Polisi yasema uchunguzi mzito
unaendelea
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imezuia
kampuni ya Said Salim Bakhresa & Co. Limited kupeleka makontena yake katika
Bandari yake Kavu (ICD), baada ya kugundulika kuwa baadhi ya makontena
yalipitishwa bila kulipiwa kodi.
Kwa mujibu wa barua ya TRA ya Novemba
17, mwaka huu, iliyosainiwa na Wolfagang Salia kwa niaba ya Kamishina wa
Forodha na Ushuru wa Bidhaa, kampuni hiyo imezuiwa kutumia bandari yake hiyo-
Namba 03 hadi kesi hiyo inayoshughulikiwa na mamlaka hiyo itakapotatuliwa.
“Unafahamu kwamba uondoaji wa bidhaa
kutoka eneo linalodhibitiwa na forodha, ambalo kodi na ushuru wa serikali
haujalipwa ni kinyume na sheria kwa mujibu wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya Usimamizi wa Forodha ya mwaka 2004 na kanuni zake kwa vile
husababisha upotevu wa mapato ya Serikali.
“Kwa sababu hiyo, imeamuriwa kukuzuia
kupeleka makontena katika bandari yako kavu kuanzia tarehe ya barua hii, hadi
suala hili litakapotatuliwa. Pande zote zinazohusika zinapaswa kutii amri hii.
“Kutokana na sababu hizo, tunasimamisha
upelekaji wa makontena katika bandari yako kavu. Usitishaji unaanza mara moja.
Hata hivyo utoaji wa bidhaa zilizopo katika bandari hiyo tajwa utaendelea,”
ilisema taarifa hiyo.
Mkurugenzi wa
Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard
Kayombo, alipoulizwa alikiri mamlaka hiyo kumwandikia barua mfanyabiashara huyo huku akisisitiza kuwa hawezi kuzungumzia kwa undani suala hilo kwa sababu lipo katika uchunguzi.
Kayombo, alipoulizwa alikiri mamlaka hiyo kumwandikia barua mfanyabiashara huyo huku akisisitiza kuwa hawezi kuzungumzia kwa undani suala hilo kwa sababu lipo katika uchunguzi.
“Ni kweli barua ile ni ya kwetu, lakini
mambo mengine bado yapo kwenye uchunguzi, huyo (Bakhersa) ni kati ya wengine
ambao tunaendelea kuwafanyia kazi na tukikamilisha tutawajulisha” alisema
Kayombo.
Kova
kutoa tamko leo
Gazeti hili lilipomtafuta Kamanda wa
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, ili kujua watu
ambao wamekamatwa kutokana na agizo la Rais Magufuli, alisema taarifa alizonazo
bado hazijakamilika.
“Leo sina chochote cha kusema bwana,
kesho (leo) nitatoa taarifa kwa vyombo vya habari ambayo ndiyo itakayofafanua
kila kitu,” alisema Kova.
Alipofanya ziara ya ghafla katika
bandari ya Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliwasimamisha kazi
baadhi ya vigogo waliohusishwa na upotevu wa makontena 349 ambayo
yameisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 80 kutokana na ukwepaji kodi na
kuagiza wengine wakamatwe.
Taarifa ambazo gazeti hili imezipata,
tayari maofisa kadhaa wa Bandari na wale wa TRA wamekamatwa kwa mahojiano
zaidi.
Wahusika hao wanaendelea kushikiliwa na
polisi huku uchunguzi wa akaunti zao pamoja na mali wanazomiliki ukifanywa.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, maofisa wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wameshaanza kuhakiki mali
za maofisa kadhaa wa mamlaka hizo.
Kutokana na hali hiyo MTANZANIA
ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba, ambaye alisema
kwa sasa bado wako kwenye uchunguzi wa watuhumiwa wa TRA walioagizwa
kuchunguzwa.
“Tupo kwenye uchunguzi mzito ambao
unakusanya mambo mengi sana na hata inaweza kuongezeka idadi ya watu. Sasa
ninachoweza kusema Watanzania watupe muda kila kitu kinakwenda sawa na tutatoa
taarifa ya uchunguzi wetu,” alisema Advera.
Bakhresa
kuchukua hatua
Kwa upande wake Kampuni ya Said Salim
Bakhresa & Co. Limited kupitia Idara ya Ushirikiano, ilieleza kuwapo kwa
ushirikiano baina yake na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika uchunguzi
unaoendelea.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kampuni hiyo
itachukua hatua dhidi ya wahusika. “Wale wote wanaohusika na upotevu huo
watachukuliwa hatua na kodi yote ya Serikali inalipwa na wamiliki wote wa
makontena yaliyo husika katika upotevu huo,” ilieleza taarifa hiyo.
Hata hivyo kampuni hiyo ilishangazwa na
taarifa za kujumuishwa katika upotevu wa makontena 349 yaliyoripotiwa hivi
karibuni kuwa yametolewa bandarini bila kulipiwa ushuru.
Novemba 27, mwaka huu Rais Dk. John
Magufuli, alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Rished Bade, muda mfupi baada ya ziara ya kushitukiza ya Waziri Mkuu, Majaliwa
Kassim Majaliwa aliyofanya Bandari ya Dar es Salaam.
Taarifa ya Ikulu iliyomnukuu Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, imeeleza kuwa hatua hiyo ya Dk. Magufuli
imechukuliwa baada ya kubaini kupitishwa kwa makontena zaidi ya 300 bandarini
bila kulipa kodi na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 80.
Baada ya kusimamishwa kazi kwa Bade,
Rais Magufuli alitangaza kumteua Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk. Philip
Mpango, kukaimu nafasi hiyo hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.
Pamoja na hali hiyo pia Rais Magufuli,
aliiagiza maofisa wote wa TRA kutosafari nje ya nchi, hadi uchunguzi dhidi yao
utakapokamilika.
Majaliwa alitangaza kuwasimamisha kazi
maofisa watano na watumishi watatu wa TRA, kutokana na upotevu wa makontena 349
yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 80.
Majaliwa alichukua uamuzi huo baada ya
kuzungumza na viongozi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) pamoja na wa TRA, ambapo pia
alimtaka Bade na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Lusekelo Mwaseba, washirikiane na
polisi kufuatilia upotevu huo na kuhakikisha fedha hizo zinapatikana na
kurudishwa serikalini.
Kutiwa jela, kukaguliwa akitangaza
uamuzi huo baada ya kufanya kikao na baadhi ya viongozi wa Serikali bandarini
hapo, waziri mkuu aliwataja maofisa waliosimamishwa kazi kuwa ni Kamishna wa
Forodha, Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Habibu
Mponezya.
“Hawa wanasimamishwa kazi. IGP ninaagiza
hawa watu wakamatwe na kuisaidia Polisi. Hati zao za kusafiria zikamatwe na
mali zao zikaguliwe kama zinaendana na kipato cha utumishi wa umma,” alisema
Majaliwa.
Maofisa wengine waliosimamishwa kazi ni
Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni
Mpande, Hamisi Ali Omari (hakutaja ni wa idara gani) na Mkuu wa Kitengo cha
Bandari Kavu (ICD In-Charge), Eliachi Mrema.
Pia aliagiza watumishi watatu wa mamlaka
hiyo wahamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani, ambao ni Anangisye
Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni ambao baadaye walitangazwa
kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yao
Hakuna maoni
Chapisha Maoni