SIKIKA YAILIPUA SERIKALI YA KIKWETE,NI KUHUSU UPUNGUFU WA DAWA,SOMA HAPO KUJUA
Wagonjwa wakisubiri tiba hospitali ya Taifa Muhimbili |
SERIKALI imetakiwa kuongeza fedha za kutosha kwa ajili ya vifaa
tiba kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa nchini
unaongezeka kufikia asilimia 80 kama inavyotarajiwa na Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN). Anaandika
Pendo Omary … (endelea).
Mbali na kuongeza fedha hizo pia
serikali kupitia Wizara za Fedha na Afya, inapaswa kuhakikisha fedha
zilizotegwa kwa ajili ya dawa muhimu na vifaa tiba zinatolewa kwa wakati ili
kupunguza uhaba wa dawa nchini.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es
Salaam na Asasi Isiyo ya Kiserikali ya SIKIKA – inayohusika na utetezi wa
masuala ya afya nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari
Irenei Kiria, Mkurugenzi wa Sikika amesema, “ Wizara ya Afya itoe mwongozo na
mikakati inayoeleweka na kuwezekana katika kutumia mapato ya afya ya
Halmashauri kwa ajili ya ununuzi wa dawa muhimu na vifaa tiba. Pia miongozo hii
iweke wazi mifumo ya uwazi na uwajibikaji”.
“Kwa takribani miaka minne iliyopita,
bajeti ya dawa muhimu za vifaa tiba imekuwa ikishuka na kusababisha ongezeko
kubwa la uhaba wa dawa muhimu huku waathirika wakuu wakiwa ni wananchi wa hali
ya chini,” amesema Kiria.
Kiria amesema mahitaji ya dawa muhimu
na vifaa tiba yameongezeka kutoka Sh. 188 bilioni mwaka 2011/2012 hadi
Sh. 577 bilioni mwaka 2014/2015 na makadirio ya Sh. 36.2 bilioni kwa mwaka wa
fedha 2015/2016.
Aidha kwa miaka ya fedha 2011/2012 na
2012/2013 kulikuwa na ongezeko kubwa kidogo la bajeti ya dawa muhimu na vifaa
tiba ambazo ni Sh. 123.4 bilioni na Sh. 80.5 bilioni ingawa hakukuwa na matokeo
chanya ya upatikanaji wa dawa.
“Makadilio ya bajeti ya mwaka
2015/2016 yameshuka kwa zaidi ya asilimia 48 kutoka katika bajeti ya mwaka
uliopita. Cha kujiuliza je hii bajeti inaendana na malengo ya BRN ya
kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu kwa zaidi ya asilimia 80 ifikapo mwaka
2016?,” amehoji Kiria.
Kuhusu kuchelewa kutolewa fedha, Kiria
amesema, hali hiyo inaathiri mfumo mzima wa ununuzi na usambazaji wa
dawa. Kwa mfano, kipindi cha miaka minne iliyopita ukiondoa mwaka wa
fedha 2012/2013 ambapo fedha yote iliyoidhinishwa ilitolewa, ni asilimia 78 tu
ya wastani wa fedha zinazoidhinishwa ndizo zimekuwa zikitolewa.
“Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
inapanga kutumia mapato mbadala kutoka fedha za uchangiaji (bima ya afya) ili
kusaidia bajeti ya dawa muhimu na vifaa tiba. Ni asilimia 20 ya watanzania
wamejiunga na mifuko hii. Hivyo mapato yake hayawezi kuziba pengo la bajeti ya
dawa katika mwaka wa fedha unaokuja.” Kiria ameongeza.
chanzo ni Mwanahalisi oline
Hakuna maoni
Chapisha Maoni