HABARI KUBWA LEO,MTOTO WA NYERERE,AMINA,NAO KIMYA KIMYA FOMU ZA URAIS,SOMA HAPO KUJUA
Balozi Amina Salum Ally |
MWANASIASA mashuhuri Visiwani Zanzibar, Balozi
Amina Salum Ally, ameandika historia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa
kuwa mwanamke wa kwanza kuchukua fomu ya kuomba uteuzi wa kuwania urais katika
uchaguzi mkuu wa Oktoba, huku akiainisha vipaumbele vyake 11. Anaandika Dany Tibason … (endelea).
Wakati Balozi Amina akifungua milango ya
uthubutu kwa wanawake, mtoto wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere
aitwaye Makongoro Nyerere naye ametinga mkoani Dodoma alasiri ya leo na
kukabidhiwa fomu katika Makao Makuu ya CCM.
Ikumbukwe kwamba,
Balozi Amina ambaye amewahi kushika nyadhifa kadhaa za uwaziri visiwani ikiwemo
wizara nyeti ya fedha, pia amewahi kujitokeza kuchukua fomu ya kuomba uteuzi wa
CCM kuwania urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kuleta mchuano mkali.
Akizungumza na
waandishi baada ya kukabidhiwa fomu yake, Balozi Amina amesema kipaumbele chake
cha kwanza ni kuwa na chombo maalum cha kusimamia masuala ya uchumi na
maendeleo ambacho kitakuwa na jukumu la kutoa ushauri wa haraka kuhusu maeneo
na aina ya uwekezaji unaohitajika.
Amesema chombo
hicho kitasaidia kuondosha ucheleweshwaji wa maamuzi ya uwekezaji, kuondoa
mikataba mibovu na ya hasara isiyo na tija kwa taifa.
“Kipaumbele kitawekwa kwa sekta zitakazochangia haraka moja kwa
moja kupunguza umasikini, kwa mfano, kilimo na viwanda, serikali itabuni njia
bora za kukuza uhusiano kati ya uwekezaji na ukuaji wa viwanda na kilimo
kuanzia wakulima na wajasiriamali wadogo wadogo hadi wakulima na viwanda
vikubwa,”amesema.
Amezitaja njia kuu
za usafirishaji kuwa itakuwa ni njia pekee ya kukuza uchumi ambazo ni pamoja na
reli, barabara, na usafiri wa baharini sambamba na maziwa huku akiahidi
kufufuliwa au kujengwa upya ili ziweze kuchangia haraka kukua kwa uchumi.
Amefafanua kuwa
Tanzania ina idadi kubwa ya wanawake ambapo takwimu zinaonesha idadi ya
wanawake wote ni takriban milioni 25 zaidi ya nusu ya watanzania
wote ambao wanahitaji kutambuliwa na kupewa fursa sawa kwa kushirikishwa
kikamilifu katika upangaji wa matumizi ya rasilimali za kitaifa.
Kwa imani ya
Balozi Amina, hilo linawezekana ikiwa wanawake watashirikishwa au kuwezeshwa
kushiriki katika mipango yote ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa hasa
katika maeneo ya kutoa maamuzi yaayogusa jamii.
Amesema
serikali yake itapigania kuondoa kasoro za mfumo dume ambao bado unachangia
kudumaza huduma za msingi kwa wanawake huku akitolea mfano pamoja na elimu ili
kuweze kupatikana maendeleo ya haraka.
“Mimi ninaamini,
kwa wingi wao, mkakati wa kumuendeleza na kuwainua kimaendeleo wanawake wa
kitanzania utakuwa ni njia nzuri pia ya kuwainua watanzania kutoka katika
ufukara wa kipato na kielimu pia,”amesema.
Kipaumbele chake
cha pili ni utoaji wa huduma za jamii kwa usawa kwa wote ikiwa takribani miaka
50 nchi imegubikwa na tatizo la huduma duni kwa jamii huku akitolea mfano wa
afya na kinga za mama na mwana ili kupunguza vifo.
Pato la Taifa
Kuhusu mgawo bora wa pato la taifa,
amesema kwa takribani miaka kumi iliyopita pato la nchi limekuwa likikua
kwa kiwango kinachoridhisha huku ukuaji wake haujaambatana na kuwaletea maisha
bora watanzania walio wengi.
“Kwangu tofauti
hiyo kubwa ya kipato katika jamii ni hatari kwa mustakbali wa umoja wa
kitaifa na amani na utulivu wa kuletea nchi yetu maendeleo.
KUa kuna kila sababu ya kimsingi inayohitaji utekelezaji wa haraka wa kuwepo
mgawo bora wa pato la taifa,” amesema.
Elimu
Balozi Amina amesema kuporomoka kwa ubora wa elimu katika ngazi
zote ni changamoto kubwa katika nchi ikiwa ni pamoja na wahitimu kukosa uwezo
au elimu ya kutosha kupata au kujiajiri wenyewe ili waweze kujikimu kimaisha.
Ameahidi kuhakikisha elimu wanayopata vijana inawawezesha katika
kukabili kikamilifu ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Utawala wa Sheria
Balozi Amina ameahidi kuweka mazingira bora ya kisheria katika
kuwezesha uwekezaji katika uzalishaji mali na kuendesha biashara na miradi
mikubwa nchini.
Amesema ili kukuza haraka ukuaji uchumi na kushinda vita dhidi ya
umaskini ni vyema kukubali kuwa mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa
uchumi wa nchi unahitaji kusimamiwa vyema kwa wawekezaji wa nje kuwekewa
mazingira mazuri.
Ukusanyaji kodi
Ameainisha kuwa takwimu za kitaifa zinaonyesha bayana kushuka kwa
ukusanyaji wa kodi nchini mwaka hadi mwaka tangu mwishoni mwa miaka ya 1990s.
Kwa mujibu wa Balozi Amina, mapungufu ambayo yamekuwa yakijitokeza
katika ukusanyaji huo yamekuwa yakileta adha nyingi kwa serikali na hata kwa
watanzania huku akitolea mfano kushuku au kukosekana kwa huduma muhimu za
kijamii.
Rushwa
Amesema rushwa, ufisadi, uwajibikaji usioridhisha na ukosefu
wa maadili ni mambo ya msingi ya kushughulikia kwa taifa linalofuata sera
ya uwazi na utawala bora na maadili mema.
Kwamba, Tanzania imeingia doa kutokana na kugubikwa na
vitendo vya ufisadi, rushwa na mapungufu makubwa ya ukosefu wa uadilifu na
uwajibikaji serikalini takriban katika ngazi zote.
“Mimi naamini, serikali ni lazima iwe inawahudumia wananchi wake
wote kwa kusimamia upatikanaji wa huduma bila ya ufisadi na vitendo vya rushwa
kwa kufanya hivyo, wananchi watakuwa na imani na serikali yao,”amesema.
Muungano
Balozi Amina ametamba kuwa, akipewa ridhaa ataendeleza mchakato wa
kupata Katiba mpya ambao ulisimamiwa na serikali ya awamu ya nne na kwamba yeye
ni muumini wa uhakika wa utawala.
Amesema kuwa Katiba bora itavusha taifa kwenda katika hali ya juu
ya maendeleo na amani na utulivu.
Lugha
Pia amegusia lugha ya Taifa akisema Kiswahili kwa ajili ya
mawasiliano ya aina mbalimbali ni moja ya tunu na nguzo zinazoliweka taifa kuwa
kwenye umoja upendo na mshikamano ambao ndio ulioupatia amani na usalama.
Ameseme kutokana na hali hiyo, Kiswahili kinatakiwa kiendelezwe
kudumishwa kama lugha ya Taifa na kwamba kutokana na kuongezeka kwa
mashirikiano ya kibiashara, kisiasa na kitamaduni kati ya Tanzania na nchi za
Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, inabidi kitumike na kisimamiwe
katika ufundishaji nyenzo ya kuwapatia vijana ajira.
Makongoro Nyerere achukua fomu
Mwanasiasa huyo, ambaye ameingia kwenye kinyang’anyiro kwa tambo
za kutaka kuwabana aliowaita “vibaka” ndani ya CCM, ametinga kuchukua fomu
akiongozana na Mzee Chifupa na kisha kuelezea ratiba ya kukusanya wadhamini
akianzia Singida na Tabora.
Amesema kuwa, atazunguka na usafiri wa gari ambalo alikopa kwenye
ubunge wa Afrika Mashariki na kwamba yeye hana uwezo wa kifedha kama wengine
huku akitamba kuwa hata waliofika Butiama kumsikiliza walijigharamia.
Kwa mujibu wa Makongoro, serikali ya CCM ina watu maarufu sana
ambao pia ni maarufu kwa kutoa na kupokea rushwa na kusababisha kushusha
heshima ya chama pamoja na kukigawa katika makundi ya ukabila na udini.
Kuhusu ilani ya chama, amesema kuna wengi waliosema akiingia
madarakani ataweka uchumi wa kati, wakulima wataacha jembe la mkono, jambo
alidai huo ni uongo kwa vile wagombea sio wanaotengeneza ilani ya chama.
Ratiba ya kesho
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM Makao Makuu, kesho saa
4:00 hadi 5:30 asubuhi, atakayekuwa wa kwanza kuchukua fomu ni Amos Siyatemi.
Kati ya saa 5:30 hadi 7:00, atachukua Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye.
Baadaye kuanzia saa 7:00 hadi 8:30 mchana, itakuwa zamu ya Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk.Mohamed Gharib Bilali, akifuatiwa na Balozi
Ally Karume kati ya 8:30 hadi 10:00 alasiri.
Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa
zamu yake itakuwa kuanzia saa 10:30 hadi 11:30 alasiri huku Dk. John Magufuli
akifunga dimba kwa siku hiyo kati ya 11:30 hadi 12:30 jioni.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni