IGP MANGU AKUTANA NA MASHEIKH WA MIKOA NCHINI
Mkuu
wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu akiwa na Mufti na Sheikh
mkuu wa Tanzania Shabani Simba na viongozi wengine wa dini ya kiislamu
wakati wakiingia katika ukumbi wa bwalo la maafisa wa Polisi
kuhudhuria kikao cha muendelezo wa kampeni ya familia yetu haina
mhalifu kilichoratibiwa na taasisi ya kiislamu ya Mwinyi Baraka. Picha
na Hassan Mdeme- wa Jeshi la Polisi
Mkuu
wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu akisalimiana na masheikh
wa mikoa na maimamu wa misikiti katika ukumbi wa bwalo la maafisa wa
Polisi wakati wa kikao cha muendelezo wa kampeni ya familia yetu
haina mhalifu kilichoratibiwa na taasisi ya kiislamu ya Mwinyi Baraka.
Picha na Hassan Mdeme- wa Jeshi la Polisi
Na Tamimu Adam – Jeshi la Polisi
Viongozi wa dini wametakiwa
kuendelea kufanya doria za kimwili na kiroho katika kuimarisha ulinzi
na usalama ndani ya jamii ikiwa ni pamoja na kuwajenga vijana katika
maadili mema na kuacha kutenda dhambi ya kujihusisha na vitendo vya
uhalifu.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu
alipokutana na viongozi wa dini ya kiislam katika ukumbi wa Bwalo la
maafisa wa Polisi Oysterbay, jijini Dar es salaam. Kikao hicho
kiliratibiwa na taasisi ya kiislamu ya Mwinyi Baraka inayoongozwa na
Sheikh Issa othuman.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mufti
wa Tanzania Shabani Simba, Katibu mkuu wa Bakwata, Kadhi Mkuu wa
Zanzibar, Masheikh wa mikoa ya Tanzania bara pamoja Maimamu wa Miskiti.
IGP Mangu alisema kuwa haijawahi
kutokea kokote duniani kwa Polisi kula njama na viongozi wa dini katika
kupambana na wahalifu na watenda dhambi, hivyo aliwaomba viongozi hao
wa dini waongeze mahubiri yenye kuwataka waumini kutenda mema pamoja na
kuongeza nguvu ya kuimarisha kamati za ulinzi na usalama katika nyumba
za kuabudia.
Naye, Mufti na Sheikh Mkuu wa
Tanzania Shaban Simba alisema kuwa dini zote zinahimiza waumini wake
kutenda mema na kujiepusha kushiriki katika vitendo viovu, hivyo
ameliomba Jeshi la Polisi kuendelea kuwakamata wale wote watakaobainika
kutenda uhalifu kwani hivi sasa uhalifu upo hata kwenye taasisi za dini.
Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa
mkoa wa Arusha Shabani Juma, wakati akitoa salamu za mkoa huo, alisema
kuwa mkoa wa Arusha kwa sasa hivi upo shwari na wa amani, hivyo ni
wajibu wetu kulinda amani tuliyonayo kwani ndio msingi wa kila kitu.
Kikao hicho ni muendelezo wa
mkakati wa Jeshi la Polisi katika kuwajengea uwezo viongozi wa dini,
ambapo viongozi hao wa dini waliazimia kwa pamoja kuendelea
kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kampeni ya kutengeneza familia
zisizo na wahalifu kupitia mahubili yao pamoja na kuendelea kuimarisha
kamati za ulinzi na usalama katika nyumba za ibada kwa rahisi ya
mawasiliano katika kuwadhibiti wahalifu.
No comments
Post a Comment