Afisa wa Polisi Amtwanga RISASI Mkewe, Kisha Ajiua.
Bastola iliyotumika katika shambulizi hilo. Picha na Sammy Kimatu wa Daily Nation.
AFISA wa Jeshi la Polisi
AFISA wa Jeshi la Polisi nchini Kenya
amemjeruhi vibaya mkewe kabla hajajiua. Tukio hilo lilijiri majira ya
saa saba unusu usiku ndani ya makazi yao huko South B, Nairobi.
Gazeti la Daily Nation la nchini humo limeripoti kuwa, kabla ya
tukio hilo askari huyo mwenye cheo cha Sajini Mwandamizi katika ofisi
za Westlands, alirejea nyumbani usiku wa manane na kuanza ugomvi na
mkewe. Taarifa zinaeleza kuwa ugomvi huo ulihusu kodi ya pango
walilokuwa wakiishi.
Sajini Mwandamizi huyo alimdai mkewe kiasi cha shilingi za Kenya
16,000 alizokuwa amempa kabla kwa ajili ya kulipia pango kwa mwezi huu
Machi. Hata hivyo, mkewe hakuweza kutoa kiasi hicho cha pesa wala kuwa
na maelezo yaliyotosheleza.
Kwa mujibu wa jirani yao, Peter Thuita, kulisikika yowe
zilizofuatiwa na mlio wa risasi majira ya saa tisa usiku kutoka nyumbani
kwa afisa huyo wa polisi.
Mkuu wa Upelelezi eneo la Makadara, Zach Nanguli amesema kuwa
afisa wake huyo alirejea nyumbani mapema isivyo kawaida lakini akiwa
tayari ameutwika kiasi cha kutosha. Kisha, akamtwanga mkewe risasi tano
ikiwa ni shingoni, mguuni, mkononi, begani na tumboni kabla mwanamke
huyo hajafanikiwa kujinusuru kwa kukimbilia nje ya nyumba hiyo. Baada ya
hapo, afisa huyo akajitwanga risasi kichwani na kufariki papo hapo.
Mwanamke huyo anayefahamika kwa jinala Janet Atieno,
alikimbizwa hospitalini Mariakani akiwa mahututi. Mwanamke huyo pia ni
afisa wa polisi akiwa na cheo cha Konstebo akihusika zaidi na ulinzi wa
majengo ya serikali katika eneo la Uhuru.
Silaha ya Sajini Mwandamizi, bastola ikiwa na risasi saba
ilipatikana katika eneo la tukio. Afisa Upelelezi amesema pia walikuta
maganda nane ya risasi zilizotumika.
Afisa huyo aliyejiua aliandika katika ukurasa wake wa Facebook muda mfupi kabla ya zahma hiyo. Aliandika;
“Lazima nifanye jambo la kijinga. Liwe liwalo. Nimechoka”.
No comments
Post a Comment