MKUU WA IGP ERNEST MANGU NA CHAGONJA WAKEMEA UHALIFU NA MAUAJI NCHINI....WADAI KUWA JESHI LA POLISI LIMEJIPANGA VYEMA KUKABILIANA NA MATUKIO HAYA
Jeshi
la Polisi Nchini litaendelea kupambana na vitendo vya ukatili wa
kijinsia na vitendo vya mauaji yanayosababishwa na Imani za kishirikina
kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya vitendo hivyo.
Hayo
yamesemwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu katika
mkutano mkuu wa maofisa wakuu waandamizi unaoendelea katika chuo cha
Taaluma ya Polisi Moshi (MPA) ukiwa na kauli mbiu isemayo “Zingatia
Weledi katika Kutoa Huduma bora kwa jamii”.
IGP
Mangu alisema kuna baadhi ya jamii zinafanya vitendo hivyo kama
tamaduni zao hivyo wao kwa kuliona hilo wataendelea kutoa elimu kwa njia
mbalimbali kwa kushirikiana na Taasisi nyingine ili kuhakikisha kuwa
vitendo hivyo vinakomeshwa hapa nchini.
“Tuendelee
kutoa elimu kwa jamii lakini pia tutaenelea kuchukua hatua kwa wote
wanaofanya makosa hayo kwa kuwa huo ni uhalifu kama ulivyo uhalifu
mwingine” Alisema IGP Mangu.
Naye
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja
amewataka Makamanda wa Polisi wa mikoa kushirikiana na Taasisi nyingine
za Serikali katika kutatua migogoro ya Ardhi ili kuipatia ufumbuzi
mapema kabla ya vurugu kutokea jambo ambalo litaendeleza usalama hapa
nchini.
Alisema
ni vyema Taasisi husika kushirikiana mapema katika kutatua migogoro
katika jamii kabla haijaleta madhara kwa kuwa iwapo hilo litafanyika
itaepusha uharibifu na gharama ambazo hutumika katika kutatua mgogoro
unapokuwa mkubwa na kusababisha vurugu.
Kwa
upande wake Kamishna wa Polisi Jamii nchini Mussa Ali Mussa alisema
wataendelea kutumia dhana ya Polisi Jamii katika kupambana na uhalifu
kabla haujatokea kwa kuwa wananchi wameonyesha mwitikio mkubwa tangu
kuanzishwa kwa dhana hiyo.
Alisema
kwa Mujibu wa Utafiti uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ufadhili wa COSTEC umeonyesha kuwa
Asilimia 70 ya watanzania wamekubali dhana ya Polisi Jamii na
wameonyesha kuikubali kwa kuwa imesaidia kupambana na uhalifu unaotokea
katika maeneo yao.
Mkutano
huo unaoendelea katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi una lengo la
kujadili na kufanya tathmini ya mafanikio yaliyofikiwa mwaka 2013 pamoja
na changamoto zilizopo katika kupambana na uhalifu na kuzipatia
ufumbuzi kwa mwaka 2014.

No comments
Post a Comment