Zinazobamba

Katiba Mpya itaje mahali pa ofisi za Muungano


Na Lauden Mwambona
Rasimu ya pili ya Katiba Mpya inapendekeza kuwapo kwa Serikali tatu ambazo ni Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Kwa sasa ni Serikali ya Zanzibar pekee ambayo haitayumba kama mambo hayo yatatokea, kwani tayari ina ofisi zake na watumishi wake.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina bendera, Bunge lake, vikosi vya ulinzi wa ndani pia taratibu zote za kukusanya mapato.
Lakini Serikali ya Tanganyika haina hata ofisi wala haijulikani makao makuu yake yatakuwa wapi. Serikali ya Tanganyika haina Katiba wala mgambo wa kusaidia kusimamia ukusanyaji kodi. Kwa sasa ni majiji ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na baadhi ya manispaa ambazo zina walinzi wake.
Kwa maana hiyo, Serikali ya Tanganyika ikianzishwa, lazima kwanza iombe msaada kwa Serikali ya Mapinduzi ili kulinda mali kwani polisi na Jeshi la Wananchi ni wa Muungano ambao nao watakuwa kwenye hekaheka za kupangiwa ofisi.
Hali kadhalika Serikali ya Muungano nayo itakuwa na kazi ngumu ya kusaka ofisi kama suala la Serikali tatu litapitishwa.
Bila shaka itabidi iangaliwe upya kuhusu matumizi ya Ikulu ya Dar es Salaam kwani Tanganyika itataka kuitumia.
Hata majengo ya vyombo vya ulinzi vilivyopo sasa hususan Jeshi la Wananchi, Polisi yatalazimika kuangaliwa upya makao makuu ya vyombo hivyo lazima yawekewe utaratibu mpya.
Kwa hali hiyo ipo haja kwa Katiba Mpya kuanisha taasisi mpya moja baada ya nyingine zitakazoundwa chini ya Serikali ya Muuungano zitakuwa wapi.
Katiba mpya itaje wazi Ofisi ya Rais wa Serikali ya Muungano itakuwa wapi pamoja na ya Makamu wa Rais na hata Baraza la Mawaziri kama inavyopendekezwa kwenye Sura ya saba kifungu cha 70.
Rasimu ya Katiba Mpya pia itamke wazi Ofisi za Waziri Mwandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa wapi kama inavyopendekezwa kwenye sura ya pili kifungu amba 99.
Zipo taasisi nyingi mpya zinazopendekezwa kuundwa kama Rasimu itapitishwa, hivyo ni jukumu la Katiba Mpya kutaja wazi ofisi za taasisi hizo zitakuwa wapi.
Kwa mfano kutakuwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali na makatibu wakuu. bora, mgunduzi n.k.
Ninachotaka kusisitiza katika makala haya ni kwamba kuwe na uwazi katika kuyaweka yote bayana ili watu waelewe kwani naamini kwamba msingi wa maendeleo ya Tanzania unategemea sana Katiba, si kitu kingine.
Wakati umefika kwa kila mtu ambaye yuko katika ardhi ya Tanzania kujiangalia kwa umakini namna gani anafanya mambo au anawaza kuhusu Katiba; ukweli ni kwamba tunapaswa kuiwaza Katiba kama ile ambayo inaweza kusaidia mabadiliko makubwa ya kimaendeleo kwa Taifa zima si chama au kundi la watu.
Wale wenzetu ambao wamepata nafasi ya kuwa wajumbe wa Bunge la Katiba, wanapaswa kufurahia fursa hiyo kwa kuiona kama ni adimu kwao na kwamba wanapaswa kusaidia kuleta maendeleo kwa Taifa, si kwao au vyama vyao kama ambavyo tunasikia baadhi ya watu wakifanya. Naamini kila mtu akiweka masilahi ya Taifa mbele, Tanzania inaweza kuwa na maendeleo ya haraka. Katiba ni kila kitu katika maisha, ni wazi kwamba tunapaswa kufanya kila tunachoweza kuhakikisha nchi yetu inakuwa na maendeleo.
Tuhakikishe tunakuwa na Katiba inayojibu kero za Watanzania, si zaidi. Mungu ibariki Tanzania! (P.T)
Chanzo:Mwananchi mtandaoni

No comments