GHARAMA YA UKARABATI WA BUNGE NI BILLIONI 8 LITAKAA SIKU 70 TU! MAJANGAZZZ!!
Rais Jakaya Kikwete akikagua Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma hivi karibuni.
Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Willam Lukuvi na kulia
ni Spika wa Bunge, Anne Makinda. Picha ya Maktaba.
KWA UFUPI
- Gharama hizo zinahusisha pia ununuzi wa viti 678, ukarabati wa paa, vifaa vya usalama
Dodoma. Kiasi cha
Sh8.2 bilioni kimetumika kufanya ukarabati mkubwa wa Ukumbi wa Bunge
pamoja na miundombinu yake kwa ajili ya shughuli za Bunge la Katiba
litakalokutana kwa zaidi ya siku 70.
Mbali ya gharama hizo, imeelezwa pia kuwa kila mbunge wa Bunge hilo
maalumu la Katiba atalipwa Sh300,000 kwa siku katika kipindi chote
litakapokuwa linakutana.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah aliwaambia waandishi habari Mjini
Dodoma jana kuwa posho hizo za wabunge zimechanganuliwa katika sehemu
mbili.
Alisema Sh220,000 ni kwa ajili ya posho ya kikao, usafiri na dereva na
Sh80,000 ni posho ya kujikimu na kwamba hicho ndicho kiwango
kilichoidhinishwa na Rais Jakaya Kikwete.
“Tuliposikia kuwa wabunge watalipwa posho ya Sh700,000 kwa siku na sisi
hatukujua ilitokea wapi kwa sababu Rais hakuidhinisha malipo ya aina
hiyo,” alisema Dk Kashililah.
Gharama za ukarabati
Kuhusu ukarabati wa ukumbi na miundombinu yake iliyogharimu Sh8.2
bilioni, Dk Kashililah alisema viti vipya 678 vilivyofungwa kwenye
ukumbi huo vimegharimu takribani Dola za Marekani milioni moja (sawa na
Sh1.6 bilioni) pamoja na gharama za usafiri.
Alisema gharama nyingine zimetokana na marekebisho ya mfumo wa sauti
ambao ulikuwa ukilalamikiwa na wabunge kutokana na kutosikika vizuri kwa
baadhi ya vipaza sauti.
Dk Kashililah alisema ukarabati huo umehusisha, mfumo mpya unaotumia
teknolojia ya dijiti na kuboresha mitambo ya Idara ya Kuhifadhia ya
Kumbukumbu Rasmi za Bunge ili iweze kuhimili idadi ya wabunge hao zaidi
ya 600.
Alisema gharama nyingine zimetokana na ukarabati wa mifumo ya kuimarisha
usalama pamoja na kuweka vioo visivyopenya risasi katika baadhi ya
kumbi.
Alisema fedha nyingine zimetumika kukarabati paa la Ukumbi wa Bunge ambalo lilikuwa linavuja.
Pia fedha hizo zimetumika kurekebisha mitambo ya kufua umeme, maji,
kuzima moto na viyoyozi na kumalizia ujenzi wa jengo ambalo litakuwa
likitumika kwa ajili ya sehemu ya mazoezi, benki na ofisi za wabunge
zaidi 100.
Dk Kashililah alisema kiasi hicho kimetumika kwa ajili ya kununua samani
za ofisi za wabunge na kuongeza eneo la mgawaha na kuboresha
miundombinu kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Alisema fedha zote zilizotumika katika ukarabati huo zimetokana na
bajeti ya mipango ya maendeleo iliyopitishwa na Bunge mwaka jana na
kwamba si jambo geni huku akisema kazi zote zimefanywa kwa mara moja.
Ratiba ya Bunge la Katiba
Kwa upande wa ratiba ya Bunge la Katiba, Dk Kashililah alisema litaanza
shughuli zake rasmi kesho kwa kusomwa kwa tangazo la kuitishwa kwa Bunge
Maalumu la Katiba la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Siku hiyo pia kutafanyika uchaguzi wa mwenyekiti wa muda ambaye kazi
yake kubwa itakuwa ni kuandaa kanuni za Bunge Maalumu la Katiba ambalo
litakuwa na wajumbe 629.
Alisema baada ya kupatikana kwa kanuni, Ijumaa kutafanyika uchaguzi wa
mwenyekiti na makamu wake kwa kuzingatia sheria ya Mabadiliko ya Katiba
iliyopitishwa mwaka jana.
Alidokeza kwa kusema pia kuwa wateuliwa, Katibu na msaidizi wake wa
Bunge hilo na kwa mujibu sheria hiyo, ataanza kazi baada ya kuapishwa na
Rais na baada ya kuapishwa naye atamwapisha mwenyekiti wa Bunge hilo.
Baada ya mwenyekiti kuapishwa, atawalisha kiapo wajumbe wengine wa Bunge
hilo, kazi ambayo itafanyika kwa siku tatu hadi Jumatatu asubuhi na
mchana wake, Rais Kikwete atalizindua rasmi.
GHARAMA YA UKARABATI WA BUNGE NI BILLIONI 8 LITAKAA SIKU 70 TU! MAJANGAZZZ!!
Reviewed by Full habari Digital
on
11:21:00
Rating: 5
Reviewed by Full habari Digital
on
11:21:00
Rating: 5


No comments
Post a Comment