NATANGULIA kuomba radhi kwa wasomaji wangu kwa kutotekeleza matakwa yao ya kuomba niweke hadharani makala ya Zitto Kabwe iliyochapishwa na gazeti hili mwanzoni mwa mwaka huu, akieleza CHADEMA ilikotoka na kufikia hapa ilipo.
Maombi ya wasomaji yalitokana na makala yangu niliyoiandika Jumatano wiki
hii ikisomeka kuwa: ‘Nitawatafakari Zitto na Dk. Kitila hadi kesho’, ambapo
nilikumbushia makala ile ya Zitto aliyokuwa akiwamwagia sifa wenyeviti wa
CHADEMA, hasa Freeman Mbowe.
Niseme kwamba nia yangu haikuwa kumwaibisha Zitto wala kuonyesha kama nimkosaji kwa tuhuma zinazomkabili bali nilitaka kuwakumbusha wasomaji kuwawanasiasa wetu ni wasahaulifu.
Hivyo, leo sikuona haja ya kuendeleza mjadala huo kwa sababu CHADEMA na
kina Zitto wako kwenye mchakato wa kumaliza suala hilo ili kurejesha imani
ya wananchi wapenda mageuzi.
Leo nataka kuwaeleza CHADEMA kuwa wana wasaliti wengi ndani ya chama ambao wanapaswa kuwabainisha hadharani mapema na kuwachukulia hatua kablahawajafanikisha nia zao ovu.
Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa bila upinzani makini
serikali inajisahau. Kwa mtu yeyote mwenye mapenzi mema na taifa hili
anapaswa kusimama wima kuhakikisha CHADEMA haiparaganyiki.
Wasomaji wengi watakubaliana na mimi jinsi wananchi walivyokata tamaa na
upinzani baada ya Augustine Mrema na wafuasi wake kudhoofisha upinzani kwa kuviua vyama vya NCCR-Mageuzi na TLP.
Bila shaka tunakumbuka serikali ya CCM ilivyokidhoofisha Chama cha Wananchi(CUF) kwa propaganda za udini na kukipunguza makali yake ya kuisimamia
serikali.
Sasa CHADEMA ndicho chama kikuu cha upinzani ambacho kimefanya kazi kubwa ya kuisimamia serikali ya CCM na kuiwajibisha kwa vitendo vya kifisadi.
Nguvu kubwa za kila namna zimetumiwa na serikali ya CCM kujaribu
kuisambaratisha CHADEMA kwa kutumia vyombo vya dola, propaganda za udini, ukabila, ukanda, siasa chafu na ugaidi lakini yote hayo yamegonga mwamba.
Wananchi wameendelea kuiamini na kuiunga mkono CHADEMA baada ya kuona imevuka vitimbi vyote hivyo.Badala yake CCM bila kujua wanaendeleza siasa chafu, bila kutambua kuwa wanaipa umaarufu CHADEMA.
Leo njama za kuwagawa watu kwa misingi ya ukabila, zimeshindikana baada ya propaganda za CCM kudai CHADEMA ni chama cha Wachaga. Udini umeshindikana baada ya tuhuma za kuihusisha CHADEMA na Ukatoliki kufeli. Mbinu iliyobaki ni kuwanunua viongozi.
Mkakati huu umeanza siku nyingi, sasa ndipo mambo yameanza kujifunua baada ya waraka wa kina Zitto, Dk. Kitila na Samson Mwigamba kubainika.
Hawa ni sehemu tu, wako wengi walishakamata mshiko na kufanya mazungumzo ya kupewa ubunge wa kuteuliwa, ukuu wa wilaya na nafasi nyinginezo serikalini
baada ya kukamilisha mkakati wa kuivuruga CHADEMA.
Kama nilivyotangulia kusema kuwa Watanzania wapenda mageuzi na nchi yao
hawawezi kukubali CHADEMA ikafa kibudu kwa sababu tu ya kuwalea wasaliti
wanaochuma rushwa kwa ajili ya matumbo yao, ukweli sasa umedhihiri,
wasaliti wasakwe popote na kutoswa.
Watu wamekufa, wamemwaga damu, wamebaki vilema kwa kipigo cha mitutu ya dola wakati wakiimarisha CHADEMA, nani anaweza leo kuendelea kuwaonea haya wala rushwa na walevi wa madaraka eti wakisambaratishe chama CCM ipumue?
Ni kweli Mbowe na Katibu wake Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, hawaiongozi CHADEMA milele, lazima wakati utafika wataondoka, lakini kwa mtu makini na mwana mageuzi asingeweza kutunga waraka wa kifisadi kuwachafua wakati wamekiletea chama mafanikio makubwa.
Kwa wasaliti wote na wapenda rushwa na vyeo vya kununuliwa na watawala ebu soma hapa kisha linganisha historia ya watu hawa. Dk. Kitila anatoka mkoani Singida katika Jimbo la Iramba Magharibi linaloongozwa na Mwigulu Nchemba. Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, sijui alikisaidiaje chama chake kupata ushindi mkoani kwake, lakini CHADEMA iliambulia jimbo moja la Singida Mashariki la Tundu Lissu na madiwani wachache sana.
Zitto alikuwa Naibu Katibu Mkuu, kati ya majimbo manane ya Mkoa wa Kigoma kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, alikiwezesha chama chake kushinda jimbo moja la kwake la Kigoma Kaskazini, lakini halmashauri yake inaongozwa na CCM.
NCCR-Mageuzi mkoani humo iliipokonya CCM majimbo manne ya Kigoma Kusini, Kasulu Mjini na Vijijini na Muhambwe, halafu CCM akaambulia Buyungu, Kigoma Mjini na Kibondo. Mbowe ambaye anatengenezewa zengwe la kuondolewa madarakani na vibaraka wa CCM, amekisaidia chama chake kupata majimbo matatu ya Hai, Rombo na Moshi Mjini pamoja na kuzoa madiwani wengi.
Hivi sasa Halmashauri yake ya Hai inaongozwa na mwenyekiti kutoka CHADEMA, Moshi Mjini inaongozwa na Meya wa CHADEMA, wakati Moshi Vijijini, CHADEMA na TLP zimegawana madaraka kwa vile zina madiwani wengi. Dk. Slaa anatoka Arusha, pamoja na kwamba aligombea urais lakini Jimbo lake la Karatu aliloliongoza kwa vipindi vitatu alifanikisha kulitetea chini y Mchungaji Israel Natse, Jimbo la Arusha Mjini ni la CHADEMA na Arumeru
Mashariki pia. Karatu kwa Dk. Slaa halmashauri hiyo tangu mfumo wa vyama vingi kurejeshwa inaongozwa na CHADEMA, Arusha Mjini ilipaswa kuwa ya CHADEMA japokuwa CC ilichakachua uchaguzi na hata majimbo ya mkoani Arusha mengine wan madiwani wengi.
Kwa mfano huo mdogo unaweza ukatafakari mwenyewe kuwa hawa wanaotaka kuchoma nyumba yao wenyewe ndani ya CHADEMA lengo lao ni kuleta mabadiliko gani?
No comments
Post a Comment