KIKONGWE ALIVYOUAWA NA KUCHUNWA NGOZI MOROGORO
Familia iliyohusika kumsaka kikongwe Helena Petri siku aliyopotea.Picha na Juma Mtanda
Morogoro. Tukio la kifo cha kikongwe, Hellan Petri Mahunzila (75) ambaye alipotea katika mazingira ya kutatanisha kwa siku 12 kisha siku ya 13 mwili wake kuonekana kando ya shamba lake huku mwili wake ukiwa imechunwa ngozi mwili mzima, imezua hofu kubwa.
Wakazi Kitongoji cha Gongo,
Kijiji cha Mgata, Kata
ya Bwakilajuu mkoani Morogoro, ambako tukio hilo limetokea, sasa
wanaishi kwa hofu.
Baadhi yao wanalazimika
kujisaidia haja ndogo na
kubwa katika makopo hasa nyakati za usiku, ndani ya nyumba zao. Tukio
hilo limebadili kabisa mfumo wa maisha na kutembea, wengi wanalazimika
kuingia ndani ya nyumba kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12:30 jioni
wakihofia kutekwa.
Tukio lenyewe
Ni saa 7 usiku, siku ya
Jumatano kuamkia Alhamisi
ya Oktoba 2 mwaka huu, Eliza Steven (19) anaamka na kumnyonyesha
kichanga chake, James Peter (miezi mitatu), baada ya kilio cha mtoto
huyo mchanga kuhitaji kunyonya.
Baada ya James kunyonya na
kushiba, alinyamaza
kulia, hiyo ilikuwa ni kama kumpa fursa mama yake kutoka ndani ili aende
nje kwa ajili ya kujisaidia haja ndogo.
Anafungua mlango wa chumba
chake na kutoka nje
kujisaidia huku akipiga jicho na kuangalia mlango wa chumba anacholala
bibi yake, anaona mlango upo wazi. Jambo hilo, hakulitilia shaka sana
kwani alikuwa na imani angeweza kukutana naye nje ama chooni, haikuwa
hivyo.
Alilazimika baadaye kuingia
chumba anacholala
bibi huyo, aliangalia kitandani ili kuweza kujibu maswali yake yaliyojaa
kichwani likiwamo la kwa nini bibi yake ameshindwa kufunga mlango kama
alitoka nje? Anaanza kusema Eliza. Eliza aliendelea kueleza kuwa baada
ya kuchunguza katika chumba kile kinachotumiwa na bibi yake, Hellen
ambaye alikuwa na kawaida ya kufunga mlango pindi aiingiapo kulala,
hakumwona na kuchukua jukumu la kumwamsha mama yake mzazi, Yustina
Kasian (40) ili aweze kusaidiana naye kumtafuta.
Yustina Kasian ambaye ni
mtoto wa pili kwa
kuzaliwa kwa bibi, Hellen Petri Mahunzila anasema baada ya kuelezwa
maneno yale na mtoto wake, Eliza Steven ambaye ni bibi yake alienda
katika kile chumba anacholala mama yake na kuangalia huku na huku, bila
mafanikio.
“Nilienda chooni na
kuangalia ndani ya choo lakini
sikumwona, nilirudi ndani na kumwamsha mume wangu, Steven Francis (50)
ili naye atusaidie kumfuata kwani tayari hofu ilianza kutanda moyoni
mwetu na kujiuliza maswali ambayo hatukuweza kupata majibu usiku ule,”
anasema Yustina.
Mimi baada ya kuelezwa jambo
hilo na mke wangu
nilitoka nje na tochi hadi chooni na kumulika ndani na kuzunguka kile
choo, sikuweza kumwona. Nilienda pia kumtafuta kwenye banda la kupikia
na eneo zima la migomba lakini mama mkwe wangu hakuweza kuonekana akiwa
hai ama amekufa,” anasema Steven Francis.
Francis anasema baada ya
kushindwa walikwenda kwa
majirani kuomba msaada wa kumtafuta; walikwenda kwa jirani Selis Silili
na Calist Stephano.
Jirani zake hao walitoa wazo
la kwenda kutoa taarifa la tukio
hilo kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Gongo, Kijiji cha Mgata, Kata ya
Bwakilajuu, Festo Mfaume usiku ule wa saa 7:45.
Mwenyekiti huyo aliwaeleza
kuwa kutokana na giza nene na mvua wangemtafuta asubuhi yake siku ya
Alhamisi.
Mwenyekiti huyo wa Kitongoji
cha Gongo, Festo Mfaume katika mahojiano na mwandishi wa makala haya
anasema,
“Kitongoji changu kina
zaidi ya wananchi 325 na
tukio hili limekuwa la kwanza kutokea. Nilichofanya ni kuwatawanya watu
katika makundi kuanza kumtafuta bibi yetu Hellen sehemu za misitu,
vichanga, shambani kwake, mapango na kutoa taarifa vitongoji vya jirani
ili nao watusaidie kumtafuta, lakini tulifanya kazi hiyo kwa siku sita
bila mafanikio na kukata tamaa”.
Katika ardhi ya kitongoji
hicho hakuna sehemu
ambayo wananchi wameshindwa kufika lakini cha ajabu baada ya wao kukata
tamaa kwa kumtafuta kwa siku sita, mwili wake ulionwa na mjukuu wake,
Eliza Steven Oktoba 15 kando ya shamba lake ukiwa umechunwa ngozi na
kutelekezwa, anasema mwenyekiti huyo wa kitongoji.
Siku ya Oktoba 15 saa 7
mchana mwaka huu, Eliza
Steven aliondoka nyumbani kwenda shambani kuchuma mbaazi katika shamba
la bibi yake, mita chache aliona nyasi zimelala na mburuzo wa kitu jambo
hilo lilimshtua.
“Kabla ya njia ya kuingilia
shambani niliona nyasi
zimelala, ni kama kuna kitu kilikuwa kimeburuzwa, nilistuka kidogo kwa
sababu eneo hilo la mburuzo kuna nyasi na miba, nami nikaona ngoja
nipite katika njia hiyo ya mburuzo nione mwisho wake,” alisema Eliza.
Eliza anasema umbali wa
hatua 18 za miguu akaona
khanga na hatua mbili mbele yake akaona tena kitenge, aliponyanyua
macho mbele yake aliona mwili wa mtu.
“Nilitambua zile nguo kuwa
ni za bibi yangu Hellen
aliyepotea siku 13 zilizopita na nilipousogelea zaidi ule mwili
nilitambua kwa kuona nguo nyingine ambazo alivalishwa likiwamo gauni,
bangili, hereni na shanga shingoni lakini mwili wake nilishangaa kuuona
umekuwa mweupe hauna ngozi”.
Baada ya kuona vile
alipatapwa na mshtuko mkubwa
huku moyo ukimdunda kwa hofu kwa kuona tukio hilo ambalo kwake ni la
ajabu na kuamua kurudi kinyumenyume huku akimwita mama yake ambaye naye
alienda shambani huko akimpelekea mtoto wake ambaye alikuwa analia ili
aweze kumnyonyesha kwani siyo mbali na shamba.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha
Gongo, Festo Mfaume
anaeleza kuwa baada ya kuonekana kwa mwili huo alifuatwa nyumbani kwake
na kijana aliyefahamika kwa jina la Anthony Kalisti na kumweleza kuwa
bibi aliyepotea ameonakana kando ya shamba lake lakini tayari amekufa.
Diwani wa Kata ya
Bwakilajuu, Emili Kidevu anasema
“Baada ya mimi kujulishwa juu ya tukio lile na kuona mwili namna
ulivyochunwa ngozi mwili mzima, nilienda Ofisi ya Mtendaji na Mwenyekiti
wa Kijiji cha Mgata kutoa taarifa. Akatoa agizo la kuulinda mwili ule
hadi atakapofanya utaratibu wa kuwaleta askari polisi na daktari ili
wachunguze tukio hilo”.
Marehemu Hellen Petri
Mahunzila (75) ameacha watoto watatu
wakiwamo wawili wa kiume , Kassim Athmani Lingila (58), Banzi Mazangwa
(55) na mwanamke pekee, Yustina Kasian (40) na aliachana na mume wake
miaka 10 iliyopita huku historia yake ikielezwa kuwa maisha yake yote
alijishughulisha na suala la kilimo.
Diwani wa Kata ya
Bwakilajuu, Emili Kidevu anasema
kuwa tangu kutokea tukio hilo hakuna uchunguzi wowote umefanyika kutoka
ndani ya jeshi la polisi zaidi ya kufika siku ya tukio.
Shaka nyingine inayumkumba
diwani huyu na jamii ya
Kitongoji cha Gongo, Kijiji cha Mgata na vijiji jirani ni namna tukio
hilo lilivyotekelezwa kiutalaamu bila kukosea. Kwanza anaweza kusema
kuwa marehemu alitekwa, kisha akahifadhiwa ndani ya nyumba kwa siku 10
kabla ya kifo chake.
Naye Kamanda wa jeshi la
Polisi mkoa wa Morogoro,
Faustine Shilogile akitolea ufafanuzi na kuthibitisha kutokea kwa tukio
la marehemu, Hellen Petro (75) kufariki dunia baada ya kupotea kwa siku
11 kisha mwili wake kukutwa umechunwa ngozi siku ya 12 amelihusisha
tukio hilo na masuala ya ushirikina.
Shilogile anasema kuwa jeshi
la polisi lipo katika
uchunguzi wa kuwabaini wauaji na watakapobainika sheria itafuata mkondo
wa sheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.
“Jeshi la Polisi linaendelea
na uchunguzi, tuna imani wahusika watakamatwa,” anasema.
MWANANCHI
MWANANCHI
Hakuna maoni
Chapisha Maoni