kazi ya kuyasaka mafisadi yaanza, watatu wahojiwa na kikosi kazi
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Freeman Mbowe, Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja na
Mfanyabiashara maarufu, Rostam Aziz, wamehojiwa kuhusu kuwa na utajiri
mkubwa nje ya nchi.
Wanasiasa hao wamehojiwa na kikosi kazi maalumu kilichoundwa
na serikali hivi karibuni kwa ajili ya kutafuta mali mbalimbali
zilizofichwa nje ya nchi na watu mbalimbai wenye nyadhifa kubwa.
Ingawa watendaji wakuu wa kikosi kazi hicho wamekataa
kuthibitisha au
kukana kuhusu kuhojiwa kwa wanasiasa hao, Raia Mwema limeambiwa wanasiasa hao ni sehemu tu ya watu zaidi ya 100
wanaochunguzwa na vyombo vya dola.
Kikosi hicho kiliundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na
kinaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema,
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
Dk. Edward Hoseah na wawakilishi kutoka Jeshi la Polisi, Benki Kuu ya
Tanzania
(BoT) na waatalamu wa masuala ya kibenki.
Chanzo cha kuaminika cha
kilisema *Mbowe* ambaye pia ndiye Kiongozi wa Upinzani Bungeni, *alihojiwa kutokana na maelezo kuwa
alinunua jumba la kifahari nchini Dubai, Desemba mwaka 2011.
“Kutokana na wadhifa wake kwa umma, Mbowe ilibidi achunguzwe
kutokana na ununuzi wa nyumba alioufanya nchini Dubai, Desemba mwaka
2011.
Uchunguzi wake ni mahususi kwa sababu tumefuatilia akaunti
zake na ikaonekana hakuwahi kutumia njia ya benki kufanya malipo.
“Hii maana yake ni kwamba kama alifanya malipo, basi
alifanya kwa kutumia fedha taslim (cash).
Sasa ni lazima ichunguzwe maana si kawaida kwa kiongozi kama
yeye kusafiri na mamilioni yote ya kununua jumba kule Dubai na
kulipa cash.Ndiyo maana yeye anafanyiwa uchunguzi mahususi,” kilisema
chanzo cha kuaminika cha gazeti hili.
Rostam ni miongoni mwa wafanyabiashara maarufu hapa nchini
na *Raia Mwema *limeelezwa kwamba alihojiwa kutokana na kumiliki
jumba katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati na imeelezwa pia kuwa ana
akaunti kadhaa nje ya nchi.
Dubai ni kimbilio la wafanyabiashara wengi kutokana na nafuu
ya kodi inayotolewa na serikali ya nchi hiyo na pia uwepo wa
biashara na usalama mkubwa uliopo.
Zaidi ya kuwa mfanyabiashara maarufu, Rostam aliwahi kuwa
mbunge kupitia chama Cha Mapinduzi (CCM) na alipata pia kuwa Mweka Hazina
wa chama hicho.
Hadi tunakwenda mitamboni, gazeti hili lilikuwa halijafahamu
ni kwa sababu ya mali zipi hasa ambazo Ngeleja anazo lakini wakati
akiwa Waziri wa Nishati na Madini, kulikuwa na minong’ono kwamba alikuwa
miongoni mwa mawaziri vijana wenye ukwasi mkubwa alioukwaa ndani ya muda
mfupi.
Alipoulizwa na *Raia Mwema* kuhusu alichohojiwa alipoitwa na
kikosi kazi, Ngeleja alijibu kwa ujumbe mfupi wa maneno kupitia
simu yake ya
mkononi; “Samahani, mimi si msemaji wa suala hilo.” Hata
alipoombwa na mwandishi walau kukanusha au kukataa kuwa alihojiwa –
Ngeleja alijibu kwa ufupi, “Ahsante.”
Kwa sasa, waziri huyo wa zamani wa serikali ya Rais Jakaya
Kikwete yuko safarini nje ya nchi.
Alipotafutwa wiki hii kueleza upande wake kuhusu
alichohojiwa, Rostam hakujibu simu wala ujumbe mfupi wa maneno aliotumiwa na
mwandishi.
Mbowe hakuwa tayari kueleza kuhusu kuhojiwa huko ingawa
Ofisa Habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, aliyeeleza kuwa ameagizwa kujibu
kwa niaba ya mkuu huyo wa upinzani, alisema; “si jambo la ajabu kwa Mbowe
kuwa na mali nje ya nchi kwa vile ni mfanyabiashara na ana biashara
hadi nje ya nchi.”
Kikosi kazi kinafanya kazi zake katika mazingira ya usiri na
tangu
kilipoanza kazi mapema mwaka huu, hakijawahi kutoa taarifa
rasmi kuhusu shughuli zake.
Mmoja wa wajumbe wa kikosi kazi hicho, Dk. Hoseah alikataa
kuzungumza chochote kuhusu watu waliowahoji kwa maelezo kuwa msemaji wa
shughuli yao ni Werema.
Werema hakutaka kukana wala kuthibitisha taarifa hii
isipokuwa katika mazungumzo ya nyuma na vyombo vya habari aliwahi kusema
kwamba ni kinyume cha maadili kwa tume hiyo kutoa taarifa kuhusu watu
iliowahoji.
*Raia Mwema* linafahamu kwamba mtu kuhojiwa na kikosi hicho
haimaanishi moja kwa moja kwamba ni fisadi isipokuwa mahojiano
yanafanyika kwa minajili ya kukusanya taarifa.
Novemba mwaka jana, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA),
Zitto Kabwe,alitoa hoja binafsi bungeni akitaka ufanyike uchunguzi wa
fedha na mali haramu kutoka Tanzania zilizofichwa katika nchi mbalimbali
duniani.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, raia wake hawaruhusiwi
kufungua akaunti katika nchi za kigeni pasipo ruhusa ya ofisi ya
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
Katika hoja yake binafsi, Zitto alitaka Bunge lipewe nguvu
ya kuunda Kamati Teule ambayo itachunguza na kubaini ni akina nani
wanamiliki akaunti na mali ughaibuni lakini serikali iliamua yenyewe
kuwa ndiyo itafuatilia kwa kutumia vyombo vyake.
-Raia Mwema
No comments
Post a Comment