Zinazobamba

SERIKALI YAONYA MAWAKALA WA AJIRA ZA NJE

Na Mussa Augustine:Dar es salaam 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na , Deus Sangu matoa maelekezo kwa Mawakala binafsi wanaotangaza nafasi za ajira nje ya nchi kuzingatia taratibu za Serikali na kupata idhini kabla ya kusambaza matangazo hayo, huku watakaokiuka wakikabiliwa na hatua za kisheria.

Waziri Sangu ametoa maelekezo hayo Novemba 5,2026 Jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya kuwaaga Watanzania wapatao 985 wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi, akisisitiza kuwa matangazo yote ya fursa hizo lazima yapitie Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha taratibu zote za kisheria zinafuatwa .

"Baadhi ya mawakala wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kutangaza nafasi za kazi bila idhini ya Serikali,jambo linaloweza kuhatarisha usalama wa vijana,hivyo mawakala hakikisheni Vijana wote wanaokwenda kufanya kazi ughaibuni wanapata mafunzo kuhusu haki na wajibu wao, mazingira ya kazi na usimamizi wa fedha."amesisitiza SanguNakuongeza kuwa "Mawakala hakikisheni mikataba imebainisha wazi mishahara, maslahi na wajibu wa mwajiri na mwajiriwa,msiwape vijana mikataba tofauti na masharti wanayokutana nayo wanapofika katika nchi husika,msitoze gharama zisizoruhusiwa,kuna baadhi ya mawakala tayari wamesitishiwa leseni zao kutokana na kukiuka taratibu za kisheria zilizowekwa na Serikali."

Katika hatua nyingine Sangu amesema mpango huo umefanikiwa kuunganisha  vijana 10,471 na ajira nje ya nchi katika kipindi cha mwaka mmoja, huku Serikali ikiendelea kufanyia kazi nafasi zaidi ya 4,000 zilizopatikana wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba, nchini Qatar.Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima, amewataka vijana hao kuwa na nidhamu, kufanya kazi kwa bidii, kuweka akiba kwa ajili ya uwekezaji na kujifunza ujuzi mwingine.

Kilima pia amewataka kuheshimu sheria za nchi wanazokwenda na kuwa makini wanapotuma fedha kwa watu wengine, akisisitiza kuwa wanaiwakilisha Tanzania.Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Robert Kadege, amewahimiza kujiunga na mifumo ya hifadhi ya jamii na kuendelea kuchangia ili kujihakikishia mafao na usalama wa kifedha hata wanapokuwa nje ya nchi.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TRAA, Abdallah Mohamed, amesema mawakala binafsi wana mchango mkubwa katika kutafuta fursa za ajira na kuwaunganisha vijana na waajiri, hivyo amewataka kuendeleza ushirikiano na Serikali kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa ili kulinda haki na maslahi ya Watanzania.



No comments