DKT.MASOUD APENDEKEZA KITENGO MAALUM KUDHIBITI MATUKIO YA WATU KUPOTEA.
Na Mwandishi Wetu.
Uundwaji wa kitengo maalum cha kushughulikia matukio ya watu kupotea na uhalifu unaohusiana na ukiukwaji wa haki za binadamu umependekezwa kuwa miongoni mwa hatua zinazoweza kuimarisha usalama wa wananchi na utawala bora nchini.
Pendekezo hilo limetolewa Oktoba 31,2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyoya kiserikali ya Everlasting Legal Aid Foundation Dkt.Khamis Masoud wakati akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dar es salaam.
Dkt.Masoud ametoa pendekezo Hilo kufuatlia kuwepo kwa malalamiko kuhusu watu kupotea katika mazingira yasiyoeleweka, hali inayotajwa kuibua hofu na mashaka miongoni mwa wananchi kuhusu usalama wa maisha yao.
"Kila malalamiko yanayohusu haki za binadamu yanapaswa kusikilizwa, kufanyiwa uchunguzi wa kina na kutolewa hitimisho kwa mujibu wa sheria, ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wahusika wote."amesema Dkt.Masoud
Ameongeza kuwa kitengo hicho kinaweza kuwa na muundo unaofanana na Kitengo cha Kudhibiti Uhalifu wa Kifedha (FCU), chini ya Makao Makuu au Mkurugenzi wa Uchunguzi na Upelelezi, kikipewa jukumu maalum la kushughulikia matukio hayo.
Aidha,vyombo vya upelelezi viimarishwe kwa kuwa na wataalamu wenye ujuzi katika masuala ya haki za binadamu na saikolojia, pamoja na kuzingatia nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yao badala ya kutegemea matumizi ya nguvu kupita kiasi.
Uchambuzi huo pia unaeleza kuwa Tanzania ina mifumo ya kijasusi na vyombo vya usalama vinavyopaswa kuhakikisha usalama wa wananchi, hivyo ni muhimu mifumo hiyo itumike kwa kuzingatia sheria na kulinda haki za kila mtu.

Kwa mujibu wa Dkt.Masoud,matumizi ya mbinu za kijasusi yanapaswa kuwa chini ya usimamizi wa sheria ili yasigeuke kuwa chanzo cha hofu na mashaka kwa wananchi.
Aidha,amesema kuwa katika mkataba wa kijamii, wananchi wameikabidhi Serikali mamlaka ya kutumia nguvu kwa niaba yao ili kuhakikisha wanalindwa. Hivyo, hali ya wananchi kuendelea kuwa na hofu kuhusu maisha na usalama wao inapaswa kuangaliwa kwa uzito.
Amehitimisha kwa kusema kuwa hatua za kuimarisha uwajibikaji, uchunguzi huru na ufuatiliaji wa malalamiko ni muhimu katika kujenga imani ya wananchi kwa vyombo vya usalama na kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa.

No comments
Post a Comment