PATUTA KUJA NA MZIZIMA FESTIVAL KUENZI TAMADUNI ZA KALE.
Na Mussa Augustine: Dar es Salaam.
Taasisi ya Pamoja Tutashinda Tanzania (PATUTA)imeandaa Tamasha lijulikanalo kama 'Mzizima Festival' ambalo shabaha yake ni kufufua,kuenzi na kurithisha Mila,desturi na Tamadunu za Kitanzania Kwa Vizazi vya sasa na vijavyo.
Akizungumza na Waandishi wa habari Oktoba 30,2026 Jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mkuu wa PATUTA Dkt.Aidan Ndaombwa amesema kuwa Tamasha hilo litafanyika kuanzia Desemba 11 hadi 13 katika viwanja vya Posta Kijitonyama Jijini Dar es salaam,nakwamba michezo mbalimbali ya jadi itafanyika pamoja na mijadala ya historia ya jiji la Dar es salaam na Maadili ya Mtanzania.
Dkt.Ndaombwa amesema kuwa Tamasha hilo litajumuisha shughuli mbalimbali za kitamaduni,michezo ya jadi,burudani na mijadala itakayowakutanisha Watanzania wa makabila,rika na umri tofauti,kwa lengo la kuwakumbusha historia ya jamii zao na maisha ya wazee wao.
"Kutakuwa na vikundi 26 vya ngoma za asili kutoka makabila mbalimbali nchini, huku waandaaji wakiwa katika mazungumzo na vikundi hivyo kwa ajili ya kuhakikisha vinashiriki."amesema Dkt.Ndaombwa
Pia amesema tamasha hilo litatoa fursa kwa vijana kujifunza michezo ya jadi kama bao,ambayo ilikuwa sehemu ya maisha ya wazee wao, pamoja na kufahamu historia ya usafiri wa umma jijini Dar es Salaam, ikiwemo chimbuko la daladala UDA na maendeleo ya usafiri wa mwendokasi.
Ameongeza kuwa historia ya Dar es Salaam kama kitovu cha biashara pia itajadiliwa,ikiwemo chimbuko na maendeleo ya Soko la Kariakoo pamoja na mchango wa wafanyabiashara kutoka maeneo na makabila mbalimbali.
"Kutakuwa na mijadala itakayowakutanisha wazee na watu waliowahi kushiriki katika shughuli za siasa,utamaduni na majeshi ili kueleza historia waliyoipitia na kuwasaidia vijana kuelewa mabadiliko yaliyotokea katika jamii."
Nakuongeza kuwa"Lengo lingine ni kukabiliana na changamoto ya kushuka kwa maadili,zamani jamii ziliishi kwa mshikamano kupitia michezo na shughuli za kitamaduni, hivyo ni muhimu kurejesha misingi hiyo kwa kuwashirikisha vijana".
Kwa upande wake Mratibu wa Tamasha hilo Mayasa Jabir,amesema Mzizima inawakilisha utamaduni wa ukarimu na historia ya Dar es Salaam,akieleza kuwa wanataka kulitumia jukwaa hilo kuitangaza Tanzania kama nchi yenye amani,fursa za kiuchumi na utamaduni unaowakaribisha wageni.
"Mzizima inahusishwa na historia ya eneo hilo na hali ya kutulia au kupoa,hivyo kupitia tamasha hilo tunataka wageni wanaotembelea Dar es Salaam waondoke wakiwa na kumbukumbu nzuri za ukarimu na amani ya Tanzania." Amesema Mayasa
Ameongeza kuwa wandaaji wa Tamasha hilo wanashirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuhakikisha tamasha hilo linafanikiwa na kuonyesha utamaduni halisi wa Tanzania.
Naye Afisa Sanaa kutoka BASATA Gabriel Awe amesema baraza hilo limeunga mkono maandalizi ya tamasha hilo baada ya waandaaji kufika ofisini kupata mwongozo kuhusu taratibu za kuandaa na kuendesha matamasha nchini.
Amesema Mzizima Festival ni jukwaa muhimu kwa sababu limegusa masuala ya utamaduni na maadili ambayo kwa sasa ni changamoto katika jamii, hususani kwa kizazi kipya kinachohitaji kufahamu namna wazee wao walivyoishi na misingi waliyokuwa wakifuata.
Ametoa wito kwa wadau na wadhamini mbalimbali kujitokeza kuunga mkono tamasha hilo ili kufanikisha malengo yake ya kuenzi utamaduni na kuunganisha vizazi.
Halikadhalika mdau wa tamasha hilo,ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji VOT AFRIKA LIMITED Bw.Everest Oende ameyahimiza makampuni na taasisi mbalimbali kutumia Mzizima Festival kama jukwaa la kuonyesha mchango wao katika shughuli za kijamii, akisema ni fursa ya sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kuhifadhi urithi wa taifa.
Amesema kampuni zinapaswa kujitokeza kuunga mkono PATUTA Organization ili tamasha hilo lifanikiwe na kuwa mfano wa ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli zinazolenga kuimarisha utamaduni wa Watanzania.




No comments
Post a Comment