MBWASI AWATAKA WAFANYABIASHARA KUJENGA CHAPA ZENYE USHINDANI
Na Mwandishi Wetu
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Robert Mbwasi, amewataka wafanyabiashara, wajasiriamali na wasanii nchini kutumia ushindani wa kibiashara kama fursa ya kuboresha bidhaa na huduma zao, kuongeza tija na kujenga chapa zinazoweza kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mbwasi alitoa wito huo akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara katika hafla ya utoaji wa tuzo za Best Brand Africa, akieleza kuwa tuzo hizo hazipaswi kutazamwa kama jukwaa la kutangaza washindi pekee, bali ni chachu ya kuhamasisha uwekezaji katika ubora, uaminifu, ubunifu, utoaji wa huduma bora na uzalishaji unaozingatia viwango.
Amesema mafanikio ya chapa zinazokubalika sokoni yanatokana na uwekezaji wa muda mrefu, uaminifu kwa wateja, ubunifu na ushindani wa haki, huku akibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na kujenga uchumi shindani unaotegemea viwanda na huduma ili kuongeza fursa za ajira.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika uzalishaji, masoko na utoaji wa huduma, akieleza kuwa ushindani wa sasa hauwezi kutenganishwa na matumizi ya teknolojia katika kukuza biashara.
Ameongeza kuwa ni muhimu kujenga na kuitangaza programu ya Made in Tanzania ili bidhaa zinazozalishwa nchini zitambulike kwa ubora, uaminifu na ubunifu, huku akiwataka wafanyabiashara kulinda haki miliki zao kwa kusajili biashara na alama za biashara kupitia taasisi husika zikiwemo BRELA na FCC.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Best Brand Africa, Zakayo Shushu, alisema jukwaa hilo limejikita katika kutambua na kuzipa heshima chapa zinazofanya vizuri sokoni na zinazopendwa na watumiaji, kwa lengo la kuwatia moyo wahusika na kuwahamasisha wengine kuwekeza katika ubora na bidii.
Shushu aliwataka vijana kuwa na subira na kuthubutu kuanzisha shughuli za biashara, akisema mafanikio hayategemei ukubwa wa mtaji pekee, bali pia uthabiti, kujituma na kujitoa katika kile wanachokifanya. Pia alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya jukwaa hilo na Serikali katika kukuza sekta ya utambuzi na upimaji wa chapa (Brand Rating).
Katika hafla hiyo, baadhi ya kampuni na wajasiriamali waliotambuliwa kwa kufanya vizuri katika maeneo yao ni pamoja na AMESCO Track Parts, ambayo Mkurugenzi wake, Amir Ali Mkuya, alipokea tuzo ya Best Brand katika upande wa Track Parts na kuwashukuru waandaaji, Serikali pamoja na wateja kwa kuendelea kuamini huduma zao.
Pia, Kampuni ya TJ World International Limited inayojihusisha na uagizaji na uuzaji wa magari, kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake, Neocleous Stemba, ilipokea tuzo hiyo huku ikieleza kuwa ushindi huo ni matokeo ya mchango wa wateja na timu nzima ya kampuni.
Washindi wengine ni Perfect Sense, ambayo tuzo yake ilipokelewa na Hamida Shafi Khan kwa niaba ya kampuni hiyo, pamoja na Cherish Us of Beauty Tanzania, ambayo Mkurugenzi wake, Susan Nangale, alitambuliwa katika vipengele vya Best Make-up Artist na Best Brand Make-up Artist Tanzania, huku akiwashukuru wateja waliompigia kura.
Nayo AJ Fashion, inayojihusisha na uuzaji wa mavazi ya wanawake, ilipokea tuzo ya Best Brand Awards kupitia mwakilishi wake, Zaynab Maganga, ambaye alisema kutambuliwa kwa kampuni hiyo ni ishara ya kuthaminiwa kwa ubora na juhudi zilizowekwa katika tasnia ya mitindo.

No comments
Post a Comment