MZEE WA MIAKA 63 AUAWA KWA PANGA, MTUHUMIWA AFARIKI KWA KIPIGO CHA WANANCHI
Na Mwandishi Wetu:Dar es salaam
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Humphrey Elisamon, maarufu kama Msoka, mwenye umri wa miaka 63, ameuawa baada ya kudaiwa kujeruhiwa kwa panga kichwani na ndugu yake mwenye umri wa miaka 22, ambaye baadaye naye alifariki dunia baada ya kushambuliwa na wananchi jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, tukio hilo limetokea Oktoba 18, 2026, katika eneo la Mungu Mwema, Hongoro, Kibamba, Wilaya ya Ubungo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Dickson Elimringi Msoka, mwenye umri wa miaka 22 na mkazi wa Hongoro, anadaiwa kumjeruhi kwa panga kichwani Humphrey Elisamon, ambaye alikuwa baba yake mkubwa.
Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alishambuliwa na wananchi kabla ya polisi kufika eneo la tukio. Alikuwa katika hali mbaya na baadaye alifariki dunia akiwa anapelekwa hospitalini.
Jeshi la Polisi limesema uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo unaendelea.
Aidha, polisi imewataka wananchi kushirikiana na mamlaka mbalimbali za kijamii, kiuchumi, kisheria na kidini katika kutatua changamoto zinazowakabili, badala ya kuchukua hatua za mkato zinazoweza kusababisha madhara makubwa.
Taarifa hiyo imetolewa Oktoba 19, 2026, na Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam.

No comments
Post a Comment