JESCA KITAMBAA CHEUPE KUTIKISA GYMKHANA NA CHIMBO LA VIJANA
Na Mwandishi Wetu:
Mfanyabiashara na Mjasiriamali maarufu jijini Dar es Salaam, Jessica Boniface Kikumbi,"Jesca Kitambaa Cheupe," amezindua hafla ya Chimbo la Vijana Branch 2026, inayofanyika katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, kuanzia Oktoba 24 hadi 25, mwaka huu.
Hafla hiyo inalenga kuwaunganisha vijana na wananchi kwa ujumla kupitia burudani, huduma za kijamii na elimu kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi zinazoweza kuwasaidia kuboresha maisha yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jesca, ambaye ni mmiliki wa kumbi za burudani na baa za Kitambaa Cheupe nchini, amesema hafla hiyo imeandaliwa ili kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali katika eneo moja, badala ya kutumia muda na gharama kuzitafuta katika maeneo tofauti.
Amesema jukwaa hilo pia litatoa fursa kwa vijana kujifunza masuala ya ajira, uwekezaji, kodi na maendeleo ya kijamii, ili kuongeza uelewa wao na kuwasaidia kutumia fursa zilizopo katika jamii.
Katika upande wa burudani, Jesca amesema hafla hiyo itahusisha ma-DJ mbalimbali pamoja na wasanii watakaowaburudisha washiriki katika siku zote mbili za tukio hilo.
Aidha, amesema washiriki watanufaika na huduma ya supu ya bure itakayotolewa kuanzia asubuhi, ikiwa ni sehemu ya shughuli zilizoandaliwa kuwavutia wananchi kuhudhuria hafla hiyo.
Mbali na burudani, hafla hiyo imewakutanisha watoa huduma na taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala ya kijamii, kisheria, kifedha na kiuchumi.
Taasisi zinazoshiriki ni pamoja na Bodi ya Mikopo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani, pamoja na taasisi za bima na watoa huduma za afya.
Pia, taasisi zinazohusika na uwekezaji zinatumia jukwaa hilo kutoa elimu kuhusu huduma zao na namna wananchi wanavyoweza kutumia fursa za kiuchumi kujiletea maendeleo.
Kupitia ushiriki wa taasisi hizo, wananchi wanapata nafasi ya kuuliza maswali, kupata ufafanuzi kuhusu taratibu mbalimbali na kufahamu huduma zinazopatikana, ikiwamo masuala ya kodi, ajira, bima na uwekezaji.
Jukwaa hilo pia linatoa nafasi kwa vijana kukutana, kubadilishana mawazo na kupata taarifa zinazoweza kuwasaidia kupanga na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
Kwa ujumla, Chimbo la Vijana Branchi 2026 linaunganisha burudani na huduma za kijamii, huku likilenga kuwafikia vijana na wananchi kwa ujumla kupitia jukwaa moja la burudani, elimu na fursa za maendeleo.


No comments
Post a Comment