CCM KIMEWEKA MIKAKATI YA KUIMARISHA USTAWI WA MAVETERANI WAKE
Na Mussa Augustine, Dar es Salaam
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeweka mikakati ya kuimarisha ustawi wa maveterani wake kwa kuanza utaratibu wa kuwawezesha kupata bima za afya, kuanzisha akaunti maalumu ya shughuli zao na kuratibu utambuzi wa maveterani katika mikoa yote nchini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti CHAMUATA Taifa, Jeremiah John Wambura, katika hafla ya kuwaenzi maveterani na kumkumbuka Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, iliyofanyika Oktoba 14, 2026, katika makao makuu ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), jijini Dar es Salaam.
Wambura amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuhifadhi historia ya Taifa, kuendeleza misingi ya umoja na kuhakikisha mchango wa waliotangulia kupigania uhuru wa Taifa na kusaidia nchi nyingi za Afrika kupata uhuru hautasahaulika.
Amesema kuwa maveterani wamekuwa na mchango mkubwa katika harakati za kupigania uhuru na wanapaswa kuendelea kuliombea Taifa na kulinda amani yake.
“Siku ya kumbukizi ya kifo cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere inapaswa kuwa fursa ya kuwaombea Watanzania na Taifa kwa ujumla ili tuendelee kuwa na amani, utulivu na mshikamano,” amesema Wambura.
Pia, amemtakia heri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akieleza matumaini yake kuwa juhudi za kuendeleza nchi zitaendelea kufanyika katika mazingira ya amani na utulivu.
Halikadhalika, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza misingi ya uongozi na uwajibikaji, akihimiza maveterani kuendelea kuwa sehemu ya juhudi za kuelimisha jamii kuhusu historia ya Taifa na umuhimu wa kulinda amani kwa vizazi vya sasa na vijavyo
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Stanley Mkandawire (MNEC), amesisitiza umuhimu wa kutambua mchango wa maveterani na kuendeleza misingi ya chama, akieleza kuwa viongozi wanapaswa kujifunza kuthamini watu walioshiriki katika historia ya Taifa.
Mkandawire amesema Mwalimu Nyerere alikuwa mtetezi wa haki na wanyonge, akichangia pia harakati za ukombozi wa mataifa mbalimbali ya Afrika. Amehimiza Watanzania kutokubali kugawanywa kwa misingi ya dini au siasa, akisisitiza kuwa wananchi wote ni Watanzania bila kujali imani zao.
Ameongeza kuwa maveterani wana wajibu wa kuendeleza elimu kuhusu historia ya Taifa, huku akiwataka vijana kujifunza misingi ya amani, umoja na mshikamano ili kuilinda Tanzania na kuendeleza maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Maveterani Mkoa wa Dar es Salaam, Yahaya Ngoma, ameeleza umuhimu wa kutambua mchango wa maveterani katika historia ya Taifa na kuhakikisha kazi zao zinaendelea kufahamika kwa vizazi vijavyo.
Aidha, Mzee Ngoma, ambaye ni muasisi wa Wimbo wa Taifa, amesema maneno yake yana uhusiano na mchango wa maveterani na harakati za kihistoria zilizohusishwa na mwaka 1953, kabla ya kuboreshwa mwaka 1964 na kiongozi wa bendi ya polisi aliyetajwa kwa jina la Mayagila.
Aidha, ameomba kuanzishwa kwa akaunti maalumu ya maveterani itakayosaidia kuratibu shughuli zao, kuwawezesha kukutana na kujadiliana kuhusu namna ya kuendeleza misingi ya umoja, upendo na mshikamano.
Pia, wamesema kuwa kuna mpango wa kuweka ofisi maalumu Dodoma kwa ajili ya kuratibu shughuli za maveterani na kuhifadhi kumbukumbu za mchango wao.
Miongoni mwa mipango iliyotajwa ni kuwatambua maveterani katika kila mkoa, kwa kuanza na angalau watatu kutoka kila mkoa ndani ya mwezi mmoja, pamoja na kuandaa mkutano wa kwanza wa maveterani kutoka nchi nzima utakaofanyika Dodoma.

No comments
Post a Comment