Zinazobamba

KILIBA ATOA WITO KODI ZA NYUMBA ZISIUMIZE WANAFUNZI

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHILISO), Geoffrey Kiliba, amewaomba wamiliki wa nyumba na wafanyabiashara wanaopangisha wanafunzi kuzingatia hali zao za kiuchumi na kuepuka kupandisha kodi kwa viwango vinavyoweza kuathiri masomo yao.

Kiliba amesema baadhi ya wamiliki wa nyumba wamepandisha kodi kutoka Sh70,000 hadi Sh150,000, hali aliyoieleza kuwa mzigo mkubwa kwa wanafunzi wanaotegemea wazazi na ndugu zao kugharamia masomo na mahitaji mengine ya maisha.

Akizungumza kuhusu changamoto zinazowakabili wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, amesema wapo wanafunzi ambao familia zao zimejitahidi kwa kuuza mifugo, mashamba na kuweka rehani mali ili kuwawezesha watoto wao kupata elimu ya juu.

Amesema kupandishwa kwa kodi kwa kiwango kikubwa kunaweza kuongeza ugumu wa maisha kwa wanafunzi na kuhatarisha safari yao ya kitaaluma, hasa wale ambao tayari wanakabiliwa na changamoto za kifedha.

“Ninawaomba wamiliki wa nyumba mtuonee huruma. Tuoneni kama watoto na vijana wenu, msipandishe kodi kwa viwango vinavyoumiza na kuathiri masomo yetu,” amesema Kiliba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Asemewe.

Ameeleza kuwa wanafunzi wanahitaji mazingira mazuri ya makazi ili waweze kuzingatia masomo yao, akiwataka wamiliki kuzingatia uwezo wa kifedha wa wapangaji wao.

Kiliba amesema kuna hosteli ndani ya vyuo na nyingine nje ya vyuo, hivyo amewataka wanaohudumia wanafunzi kwa kuwapatia makazi kuzingatia mchango wao katika kuwawezesha vijana kukamilisha elimu yao.

Amehitimisha kwa kusema wanafunzi wanahitaji ushirikiano kutoka kwa jamii inayowazunguka ili waweze kukabiliana na gharama za maisha na kuhitimu masomo yao kwa mafanikio.

No comments