Zinazobamba

DC MPOGOLO ATOA WITO KWA KANISA LA KMT KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUHAMASISHA USAFI


Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, ameliomba Kanisa la Mennonite Tanzania (KMT) kushirikiana na Serikali katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa usafi na utunzaji wa mazingira.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, katika Ibada Takatifu ya Kumweka Wakfu Askofu John Jumanne Wambura. Ibada hiyo ilihudhuriwa na mamia ya waumini, viongozi wa dini kutoka makanisa mbalimbali na viongozi wa Serikali.Mgeni Rasmi katika ibada hiyo alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyewakilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu. Mhe. Sangu aliwasilisha salamu za Rais kwa Askofu Mteule na Kanisa la Mennonite Tanzania, akiwatakia mafanikio katika utumishi wao wa kiroho.

Akizungumza katika ibada hiyo, Mhe. Mpogolo alisema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa KMT katika kujenga amani, umoja na maadili mema katika jamii. Aliwashukuru viongozi wa kanisa hilo kwa kumwalika Rais na kulichagua Jiji la Dar es Salaam kuwa mwenyeji wa tukio hilo muhimu la kiroho.Aidha, aliwataka viongozi wa KMT na taasisi nyingine za dini kutumia majukwaa yao kuelimisha waumini na jamii kuhusu umuhimu wa usafi, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mtu na unapaswa kuanzia katika maeneo ya ibada, majumbani, maeneo ya biashara na maeneo ya umma.

“Naomba Kanisa lishirikiane na Serikali katika kampeni ya kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa usafi. Usafi si jukumu la Serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mmoja wetu. Tunahitaji kuhamasisha wananchi kuepuka utupaji holela wa taka na kujenga utamaduni wa kufanya usafi kila siku,” alisema Mhe. Mpogolo.Mhe. Mpogolo pia alilishukuru Kanisa kwa kuendelea kuliombea Taifa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wa nchi. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini katika kudumisha amani, mshikamano, uwajibikaji wa wananchi na ustawi wa jamii.



No comments