BoT YABAKIZA RIBA ASILIMIA 6.25,YATOA TATHMINI YA UCHUMI
Na Mussa Augustine:DAR ES SALAAM.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kubakiza kiwango cha riba ya Benki Kuu (CBR) kuwa asilimia 6.25 kwa robo mwaka inayoishia Desemba 2026, ikisema hatua hiyo itaendelea kusaidia kudhibiti mfumuko wa bei na kuwezesha ukuaji wa uchumi.
Taarifa hiyo umetolewa leo Oktoba 8,2026 na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) Emmanuel Tutuba wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wadau wa sekta za fedha.
Tutuba amesema uamuzi huo ulifikiwa Oktoba 7,2026, na Kamati ya Sera ya Fedha (MPC), ambapo imeeleza kuwa kiwango hicho kinaendelea kuwa mwafaka katika mazingira ya sasa na kinatarajiwa kusaidia mfumuko wa bei kubaki ndani ya lengo la muda wa kati la asilimia tatu hadi tano.
Amesema licha ya changamoto zinazotokana na mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati, kupanda kwa bei za mafuta duniani na uwezekano wa athari za El Niño, hatua za kisera zinazochukuliwa na Serikali pamoja na msimamo wa sera ya fedha zinaendelea kusaidia uchumi kustahimili misukosuko hiyo.
"Katika uchumi wa dunia, Kamati imebaini kuwa mzozo wa Mashariki ya Kati umeathiri shughuli za kiuchumi na minyororo ya usambazaji wa mafuta na mbolea. Bei ya mafuta katika soko la dunia imeendelea kuwa zaidi ya dola 100 za Marekani kwa pipa, hali inayoongeza shinikizo la bei za bidhaa na huduma."amesema Tutuba
Nakuongeza kuwa"Kutokana na hali hiyo, IMF imepunguza makadirio ya ukuaji wa uchumi duniani mwaka 2026 kutoka asilimia 3.5 hadi asilimia tatu, huku Benki ya Dunia ikipunguza makadirio yake kutoka asilimia 2.9 hadi asilimia 2.5."
Amesema kwa upande wa Tanzania,uchumi umeendelea kuwa imara,takwimu zilizoboreshwa zinaonyesha kuwa Tanzania Bara ilikua kwa asilimia 6.6 katika robo ya kwanza ya 2026, huku ukuaji wa zaidi ya asilimia sita ukikadiriwa katika robo zilizofuata, ukichochewa na huduma za kifedha, uzalishaji viwandani, uwekezaji katika miundombinu na huduma za kijamii.
Amesema kwa upande wa Zanzibar uchumi ulikua kwa asilimia 6.7 katika robo ya kwanza ya 2026, huku ikikadiriwa kukua kwa zaidi ya asilimia saba katika robo zilizofuata, ikichochewa zaidi na shughuli za utalii, ujenzi na miradi ya umwagiliaji.
Aidha amesema wakati huo huo, zoezi la mapitio ya takwimu za Pato la Taifa lililofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Takwimu Kuu ya Serikali ya Zanzibar limeongeza thamani ya GDP ya Tanzania Bara.Mwaka wa msingi umebadilishwa kutoka 2015 hadi 2019, na kusababisha GDP ya Tanzania Bara mwaka 2025 kufikia Sh234.1 trilioni, sawa na Dola za Marekani bilioni 92.3, kutoka Sh230.07 trilioni zilizokadiriwa awali.
Ambapo kwa Zanzibar, GDP imefikia Sh9.2 trilioni, sawa na Dola za Marekani bilioni 3.6, kutoka Sh7.03 trilioni zilizokuwa kwenye takwimu za awali. Taasisi hizo pia zimeoanisha takwimu za hesabu za Taifa ili kuwezesha uandaaji wa GDP na viashiria vingine vya kiuchumi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Gavana Tutuba amesema katika sekta ya fedha, mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kukua kwa kasi na kufikia wastani wa asilimia 32.5 katika robo iliyoishia Septemba 2026, kiwango kilichoelezwa kuwa cha juu katika historia ya Tanzania.BoT imepongeza benki na wadau wa sekta ya fedha kwa kuwezesha upatikanaji wa mikopo hiyo kwa watu binafsi na kampuni.
Amebainisha kuwa sekta ya nje imeendelea kuwa imara licha ya changamoto za kimataifa.Nakisi ya akaunti ya kawaida ilifikia asilimia 2.5 ya GDP katika mwaka ulioishia Septemba 2026, huku mauzo ya dhahabu, mapato ya utalii na bidhaa zilizotengenezwa nchini yakisaidia kupunguza athari za ongezeko la uagizaji na gharama za usafirishaji.
Halikadhalika Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa zaidi ya Dola za Marekani bilioni sita, kiwango kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi 4.3, zaidi ya kiwango cha chini cha kitaifa cha miezi minne.
BoT imesema itaendelea kufuatilia kwa karibu mzozo wa Mashariki ya Kati na hatari zinazoweza kutokana na El Niño, huku ikiwa tayari kutumia nyenzo za sera ya fedha endapo shinikizo la mfumuko wa bei litaendelea au kuenea zaidi.
Mkutano mwingine wa Kamati ya Sera ya Fedha umepangwa kufanyika Januari 6, 2027, huku tangazo la uamuzi kuhusu kiwango cha CBR kwa robo ya kwanza ya mwaka 2027 likitarajiwa kutolewa Januari 7, 2027.

No comments
Post a Comment