NCAA, HESLB WAZINDUA MFUKO WA MASOMO KWA VIJANA WA NGORONGORO
Na Mussa Augustine.
Vijana wanaotoka katika jamii zinazoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wamepata fursa mpya ya kujiendeleza kielimu baada ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuzindua Ngorongoro Scholarship Fund, mfuko maalumu wa kufadhili elimu ya juu na elimu ya kati.
Akizungumza Agost 4,2026 na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, alisema mfuko huo unatekeleza makubaliano yaliyosainiwa Januari mwaka huu kati ya HESLB na NCAA, sambamba na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yanayozihimiza taasisi za umma kushirikiana kuboresha huduma kwa wananchi.
Amesema hatua hiyo pia ni utekelezaji wa mapendekezo ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), yaliyokuwa yakitaka HESLB kuendelea kutafuta vyanzo mbadala vya fedha za kufadhili wanafunzi wa elimu ya juu.
Dkt. Kiwia amesema HESLB imekamilisha mwongozo unaobainisha vigezo, masharti na utaratibu wa kuwapata wanufaika wa mfuko huo, pamoja na mfumo wa kidijitali wa kupokea na kuchakata maombi.
Amebainisha kuwa dirisha la kwanza la maombi litafunguliwa Agosti 15, 2026, huku wazazi, walezi na vijana wanaostahili wakitakiwa kujisomea mwongozo huo kabla ya kuwasilisha maombi.
Aidha, amesema HESLB kwa kushirikiana na NCAA itaendesha kampeni za uhamasishaji katika maeneo ya Ngorongoro ili kuhakikisha walengwa wanafahamu utaratibu wa kuomba na kunufaika na ufadhili huo.
Kwa upande wake, Meneja wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa NCAA, Gloria Bideberi, alisema mfuko huo ni sehemu ya mkakati wa kuwekeza katika rasilimali watu kwa kuamini kuwa maendeleo ya uhifadhi yanaenda sambamba na maendeleo ya wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi.
Amesema kupitia ushirikiano huo, watoto wote wanaotoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro watakaokidhi vigezo watapata nafasi ya kuendelea na masomo yao kupitia mfumo endelevu wa ufadhili.
Bideberi Amesema kwa zaidi ya miaka 30, NCAA imeendelea kugharamia elimu ya watoto wanaotoka ndani ya hifadhi, ambapo hadi mwaka wa fedha 2025/26 zaidi ya wanafunzi 15,000 wamenufaika katika fani mbalimbali zikiwemo udaktari, ualimu, uhandisi, uhasibu, uhifadhi na nyingine zinazochangia maendeleo ya taifa.
Ameongeza kuwa katika hatua ya mwanzo, mfuko huo utatoa kipaumbele kwa wanafunzi watakaosomea taaluma za uhifadhi wa wanyamapori, misitu, malikale na utalii, huku ukitarajiwa kupanuliwa kadri rasilimali zitakavyoongezeka.

No comments
Post a Comment