ZAIN FOUNDATION YATOA AJIRA, YAWAINUA VIJANA KIUCHUMI KEKO.

Diwani Ismail Amanzi akionesha baadhi ya dawa za asili zinazozalishwa na Taasisi ya Zain Foundation.
Na Mussa Augustine.
DAR ES SALAAM:
Taasisi ya Zain Foundation iliyopo katika kata ya Keko Manispaa ya Temeke imeanza kuonyesha matokeo baada ya kuwapatia ajira vijana na kuanzisha programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofini kwake Julai 30,2026 Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Keko Ismail Saidi Amanzi,amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa, huku vijana wakianza kunufaika kupitia ajira na fursa nyingine za maendeleo.
Amesema hadi sasa vijana 10 wameajiriwa moja kwa moja, huku taasisi hiyo ikiwa na dhamira ya kuwainua vijana ili waweze kujitegemea badala ya kutegemea wengine.
"Lengo letu ni kuona vijana wanajitegemea kiuchumi na wanakuwa na uwezo wa kuendesha maisha yao wenyewe.Hatutaki wawe tegemezi, bali wawe wazalishaji na wachangiaji wa maendeleo ya jamii," amesema Amanzi.
Amesema Zain Foundation imeanzishwa kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi kupitia uwezeshaji wa kiuchumi na kijamii, akiwataka wakazi wa Keko kushiriki na kuunga mkono shughuli za taasisi hiyo ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.
Amanzi amesema kata ya Keko imechaguliwa kuwa eneo la kuanzia kwa makusudi ili wananchi wake wawe wa kwanza kunufaika na huduma zinazotolewa na kampuni yao ya nyumbani kabla ya kupanuliwa katika mikoa mingine nchini na baadaye katika nchi saba ambako Zain Company tayari inafanya shughuli zake
Diwani Ismail Amanzi akionesha Moja ya dawa ya asili inazozalishwa na Taasisi ya Zain Foundation.
Mbali na kutoa ajira, amesema taasisi hiyo imeanza kutekeleza programu za kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana kwa kuwapatia huduma za kurekodi bure wanaotaka kuingia katika tasnia ya maudhui na burudani.
Pia,ujenzi wa kituo cha mazoezi (gym) unaendelea ili kuongeza fursa za maendeleo kwa vijana.
Amesema hatua hizo zitasaidia kuwahamasisha vijana kushiriki katika shughuli halali za uzalishaji,kupunguza vitendo vya uhalifu na kuongeza mchango wao katika kulinda amani na maendeleo ya Keko, Temeke na taifa kwa ujumla.
Amefafanua kuwa kwa sasa, Taasisi hiyo ina matawi matano katika Kata ya Keko, ambapo kila tawi limeanza na vijana 10, hivyo kufanya jumla ya vijana 50 wanaonufaika na programu mbalimbali za taasisi hiyo, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kadri shughuli zinavyozidi kupanuka.
Aidha, Amanzi amesema Taasisi hiyo inazalisha zaidi ya bidhaa 150 za dawa za asili zinazosaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za afya, zikiwamo magonjwa ya figo, kisukari, tezi dume, vidonda vya tumbo, malaria, pumu na maradhi mengine
Diwani Ismail Amanzi akionesha Moja ya dawa ya asili inazozalishwa na Taasisi ya Zain Foundation.
Amesema matarajio ya taasisi hiyo ni kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa kuwawezesha kujenga maisha bora, kujitegemea na kujinasua na umaskini kupitia fursa mbalimbali za kiuchumi.
Hizi ni baadhi ya Dawa za asili zinazozalishwa na Taasisi ya Zain foundation kwa ajili ya matibabu kwa binadamu.

No comments
Post a Comment