Zinazobamba

UMALITA YAZINDUA TAMASHA LA 'VITUMBUA FESTIVAL'

Na Mussa Augustine 

Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) umetangaza kuanzisha tamasha la Vitumbua Festival litakalofanyika Julai 30, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, kuanzia saa 12:00 asubuhi.

Tamasha hilo linalenga kuinua hadhi ya wachoma vitumbua, kuongeza thamani ya biashara hiyo na kutambua mchango wao katika kukuza uchumi na kutengeneza ajira.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa UMALITA Taifa, Avijawa Omary (Afidhal Omari Tebani), alisema tamasha hilo litawakutanisha wachoma vitumbua kutoka wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam watakaoshindana kuonyesha ubora wa kazi zao.

Alisema washindi wataondoka na zawadi mbalimbali, ambapo mshindi wa kwanza atajishindia fedha taslimu, kiwanja pamoja na eneo maalumu la kuendeshea biashara yake ya vitumbua.

Aidha, washindi wa pili na wa tatu watapata fedha taslimu, vifaa vya biashara na zawadi nyingine zenye lengo la kuwawezesha kuendeleza shughuli zao.Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UMALITA, Johajulieth Madata, alisema tamasha hilo pia litakuwa jukwaa la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wachoma vitumbua.

Alisema washiriki watapatiwa elimu ya matumizi ya gesi ya kupikia (LPG) badala ya kuni na mkaa ili kulinda afya, mazingira na kuboresha usafi pamoja na kuongeza tija katika uzalishaji wa vitumbua.Baadhi ya wachoma vitumbua wameeleza kuwa tamasha hilo litawapa fursa ya kutangaza biashara zao, kubadilishana uzoefu na kuongeza wigo wa masoko huku likitambua mchango wao katika uchumi wa taifa.


No comments