Zinazobamba

Muhimbili: Wengi Wafika na Homa ya Ini Imechelewa


Na Mussa Augustine 

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imesema wagonjwa wengi wa homa ya ini nchini hufika hospitalini wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa, hali inayopunguza nafasi ya matibabu kuwa na mafanikio makubwa.

Kutokana na hali hiyo, hospitali hiyo kwa kushirikiana na Mega We Care Tanzania Limited imeanzisha kampeni ya siku mbili ya uchunguzi, chanjo na elimu kuhusu homa ya ini bila malipo, inayofanyika katika IDC Clinic karibu na Kituo cha Reli ya Kisasa (SGR), jijini Dar es Salaam.

Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Ini wa Muhimbili, Dkt. Swaleh Kitabu Pazi, alisema huduma hizo zimepelekwa katikati ya jiji ili kuwafikia wananchi wanaoshindwa kwenda hospitalini kutokana na shughuli zao za kila siku.

Alisema kwa sasa kliniki ya homa ya ini ya Muhimbili inahudumia zaidi ya wagonjwa 5,000 waliosajiliwa, huku wastani wa wagonjwa 100 wakifika kila siku kwa ajili ya matibabu na ufuatiliaji.

"Tunahitaji wananchi wajenge utamaduni wa kupima afya zao mapema. Homa ya ini ikigundulika kwa wakati, madhara makubwa yanaweza kuzuilika," alisema Dkt. Pazi.

Alieleza kuwa homa ya ini aina ya B huambukizwa kupitia mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito au kujifungua, kujamiiana bila kinga, kuongezewa damu isiyo salama na matumizi ya vifaa vyenye ncha kali kwa pamoja.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa ugonjwa huo hauambukizwi kwa kushikana mikono, kuishi pamoja, mate wala jasho, akiwataka wananchi kuacha kuwanyanyapaa waathirika.

Kwa mujibu wa Dkt. Pazi, zaidi ya watu milioni 500 duniani wanaishi na virusi vya homa ya ini, huku takribani watu milioni 1.3 wakifariki kila mwaka kutokana na madhara ya homa ya ini aina ya B na C.

Alisema homa ya ini aina ya B inaweza kuzuilika kwa chanjo, wakati aina ya C inaweza kutibika endapo itagundulika mapema na mgonjwa kuanza matibabu kwa wakati.Afisa Habari wa Mega We Care Tanzania Limited, Mengi Ntasimba, alisema kampuni hiyo imechangia vifaa vya uchunguzi, chanjo na dawa kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma za kinga na matibabu kwa wananchi.

Naye Joseph Daniel Chengula, mkazi wa Kimara Mwisho, aliwataka wananchi kujitokeza kutumia fursa hiyo ya huduma za bure, akisema uchunguzi wa mapema unaweza kuokoa maisha.Wataalamu wa afya wameendelea kuhimiza wananchi kupima afya zao mara kwa mara na kupata chanjo ili kupunguza maambukizi pamoja na vifo vinavyotokana na homa ya ini.

No comments