Zinazobamba

TBA Yatikisa Sabasaba, Yatwaa Tuzo ya Banda Bora na Kuibua Fursa za Uwekezaji

Na Mussa Augustine 

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeibuka mshindi wa nafasi ya pili katika kipengele cha Banda Bora upande wa Sekta ya Miliki na Real Estate kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yaliyohitimishwa leo jijini Dar es Salaam.

Tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud W. Kondoro, na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TBA, Bi. Amina Lumuli, ambaye alisema mafanikio hayo yametokana na ubunifu uliotumika katika maandalizi ya banda la taasisi hiyo pamoja na namna lilivyofanikiwa kuwasilisha fursa mbalimbali za uwekezaji kwa wananchi na wadau wa maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Bi. Lumuli alisema TBA ilitumia maonesho hayo kuhamasisha uwekezaji kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), huku ikitoa elimu kuhusu miradi ya kimkakati inayotekelezwa na wakala huo katika maeneo mbalimbali nchini.

Alieleza kuwa wageni wengi waliotembelea banda la TBA walivutiwa na miradi mbalimbali inayotekelezwa na taasisi hiyo, ikiwemo ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, majengo ya serikali pamoja na ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya michezo, hususan Uwanja wa Benjamin Mkapa. Miradi hiyo imeendelea kudhihirisha uwezo wa TBA katika sekta ya ujenzi na usimamizi wa majengo.Bi. Lumuli alisema tuzo hiyo ni uthibitisho wa imani kubwa ambayo wananchi na wadau wanaendelea kuiweka kwa TBA kutokana na ubora wa huduma zake, ubunifu wa kihandisi na uwezo wa kutekeleza miradi yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa. Aidha, aliwahimiza wawekezaji kujitokeza na kutumia fursa zilizopo kupitia miradi ya ubia inayoratibiwa na taasisi hiyo.

Sherehe za kufunga Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba pamoja na utoaji wa tuzo ziliongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Katika maonesho hayo, TBA iliendelea kujipambanua kama miongoni mwa taasisi za serikali zinazofanya vizuri katika utoaji wa huduma, ubunifu wa kihandisi na kuvutia uwekezaji nchini.

No comments