Zinazobamba

STEVE NYERERE KUWAONGOZA MASTAA KWENYE DUA MAALUM YA KUWAOMBEA WALIOTANGULIA MBELE YA HAKI

Mwenyekiti wa taasisi ya Ongea na Mwanao, Steve Nyerere, kesho anatarajiwa kuwaongoza wasanii, wanamichezo, waandishi wa habari na Watanzania wengine katika dua maalum ya kuwaombea waliotangulia mbele ya haki.

Akizungumza leo Julai 31, 2026, jijini Dar es Salaam, Steve amesema dua hiyo itaanza asubuhi na itaongozwa na masheikh pamoja na wachungaji, huku akiwakaribisha Watanzania kujitokeza kushiriki tukio hilo la kuombea, kuwakumbuka na kuwaenzi waliotangulia.

"Kesho tutawakumbuka wasanii, wanamichezo, waandishi wa habari na viongozi waliotangulia mbele ya haki. Tunawaomba Watanzania wajitokeze tushiriki pamoja," amesema Steve.

Katika kuelekea tukio hilo, Steve pia amewataka vijana kuendelea kulinda amani, umoja na mshikamano wa Taifa.

Msanii Nyoshi El Saadat amesema dua hiyo ni jambo la kupongezwa na kuwataka Watanzania kushiriki kwa wingi.

Naye Abdallah Mkumbila maarufu kama Muhogo Mchungu amesema kuwaombea waliotangulia mbele ya haki ni jambo jema, huku Ally Choki akieleza kuwa siku hiyo itakuwa ya baraka na kuhimiza wananchi kujitokeza.

Kwa upande wake, Andrew Sekidia amesema waliotangulia wameacha msingi wa amani unaowezesha Watanzania kuendelea kutekeleza majukumu yao, hivyo ni muhimu kuendelea kuwaenzi.

Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania, Salum Abdul 'Chiky', amesema wasanii wataungana kesho katika dua hiyo, akiamini itakuwa fursa ya kuwaombea wenzao waliotangulia mbele ya haki na kuimarisha mshikamano ndani ya tasnia.

No comments