MFUMO WA ONE STOP CENTER UMEONGEZA UFANISI WA UTOAJI HUDUMA KWA WANANCHI:DKT.SEIF
Na Mussa Augustine
Mfumo wa One Stop Center ulioanzishwa katika banda la Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) umeongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa kuwawezesha wananchi kupata huduma na ufumbuzi wa changamoto zao sehemu moja.
Kauli hiyo imetolewa Julai 10,2026 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafar Seif baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu, akieleza kuwa mfumo huo umeondoa ulazima wa wananchi kutembelea halmashauri na taasisi mbalimbali kufuatilia huduma zinazotolewa na TAMISEMI.
"Ndani ya banda moja mwananchi anapata huduma nyingi kwa wakati mmoja. badala ya kwenda halmashauri moja hadi nyingine au ofisi mbalimbali, hapa anapata maelezo, ufumbuzi wa changamoto zake na, pale inapohitajika, anaunganishwa moja kwa moja na wataalamu waliopo katika maeneo husika," amesema Seif
Nakuongeza kuwa"Wataalamu kutoka idara na taasisi mbalimbali za TAMISEMI wanatoa ushauri na ufafanuzi kuhusu masuala ya elimu, uhamisho wa watumishi, ujenzi, vibali na huduma nyingine zinazotolewa na mamlaka za serikali za mtaa."
Aidha amebainisha kuwa mbali na huduma hizo,pia wananchi wanapata elimu na ushauri kutoka taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu zinazoshughulikia hifadhi ya jamii, watu wenye ulemavu, udhibiti wa dawa za kulevya pamoja na huduma nyingine za kijamii.
Amefafanua kuwa ushiriki wa Ofisi ya Waziri Mkuu katika Maonesho ya Sabasaba unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu majukumu ya taasisi zake na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka.
"Wananchi watumie siku zilizobaki za maonesho haya kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu ili kupata huduma,elimu na ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu TAMISEMI na taasisi zake."amesema

No comments
Post a Comment