Zinazobamba

BoT Yaahidi Kuendelea Kutekeleza Sera Madhubuti za Fedha Kuimarisha Uchumi


Na Mussa Augustine

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema itaendelea kutekeleza sera madhubuti za fedha ili kuhakikisha uchumi wa Tanzania unaendelea kuwa imara na wenye utulivu.

Kauli hiyo imetolewa leo, Julai 10, 2026, na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, alipotembelea banda la BoT katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba), jijini Dar es Salaam.

Tutuba amesema BoT itaendelea kuhakikisha kiwango cha mfumuko wa bei kinabaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5, huku ukwasi ukiendelea kuwepo kwa kiwango kinachowezesha ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Aidha, amesema Maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wananchi kupata elimu ya kifedha, huduma mbalimbali na taarifa kuhusu mchango wa Benki Kuu katika maendeleo ya uchumi wa taifa.Ameongeza kuwa BoT imeridhishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi wanaotembelea banda lake kupata elimu kuhusu sera za fedha, usimamizi wa sekta ya fedha, huduma ya kushughulikia malalamiko kupitia mfumo wa Sema na BoT, pamoja na fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.

"Tumeona wananchi wengi wana hamu ya kuelewa namna Benki Kuu inavyosimamia uchumi, hususan kuhusu kiwango cha riba ya Benki Kuu ambacho kwa sasa ni asilimia 6.25," amesema Tutuba.

Ameongeza kuwa tathmini ya BoT inaonesha kiwango hicho kitaendelea kusaidia kudhibiti mfumuko wa bei, kuongeza ukwasi katika mabenki na kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi.

"Tathmini yetu inaonesha kiwango hicho kitaendelea kudhibiti mfumuko wa bei, kuongeza ukwasi katika mabenki na kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi," amesema.Kuhusu thamani ya fedha, Tutuba amesema matarajio ya BoT ni kuona shilingi ya Tanzania ikiendelea kuwa imara, hususan katika kipindi cha mavuno, hali itakayowasaidia wakulima kupata bei stahiki za mazao yao na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Katika hatua nyingine, Gavana huyo amesema BoT inaendelea kukamilisha maandalizi ya sheria na kanuni zitakazosimamia mali za kidijitali, ikiwemo sarafu za kidijitali kama Bitcoin na Stablecoins, kwa lengo la kulinda watumiaji wa huduma za kifedha na kuzuia matumizi ya teknolojia hiyo katika utakatishaji wa fedha haramu pamoja na ufadhili wa ugaidi.

Amesema hatua hiyo inachukuliwa kwa kuzingatia uzoefu wa kimataifa, baada ya BoT kushiriki mijadala mbalimbali kuhusu usimamizi wa mali za kidijitali.Akizungumzia mfumo wa Sema na BoT, Tutuba amesema mfumo huo umeendelea kupunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko kutoka kwa watumiaji wa huduma za kifedha, huku BoT ikiendelea kuuboresha ili kuwafikia hata wananchi wasioweza kutumia teknolojia za kidijitali.

Hata hivyo, amewahimiza wananchi wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba kutumia fursa hiyo kutembelea mabanda mbalimbali ili kupata elimu ya kifedha na taarifa zitakazowasaidia kuboresha shughuli zao za kiuchumi.

Aidha, amesema maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania yameonesha mafanikio makubwa ya taasisi hiyo katika kuimarisha utulivu wa uchumi, usimamizi wa sekta ya benki, mifumo ya malipo, elimu ya fedha na upatikanaji wa huduma za kifedha nchini.

"Mafanikio haya yameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi tulivu na mfumo imara wa kifedha unaovutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi," amesema Tutuba.

No comments