TRA KUWEKA MAZINGIRA RAFIKI KWA WAFANYABIASHARA ILI WALIPE KODI KWA HIARI.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema itaendelea kuboresha huduma kwa wateja na kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara ili kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari nchini.
Akizungumza leo, Juni 29, 2026, katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya TRA pamoja na hafla ya Tuzo ya Rais kwa Mlipa Kodi Bora, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alisema lengo la mamlaka hiyo ni kujenga uhusiano mzuri na walipakodi badala ya kuonekana kama mnyonyaji.
"Tutaendelea kuimarisha huduma kwa wateja. Mlipakodi ndiye mfalme, lakini si mfalme wa kukimbia. Tunataka nyinyi mtukimbilie badala ya kutukimbia," alisema Mwenda.
Ameeleza kuwa licha ya Tanzania kuwa na zaidi ya watu milioni 60, bado si wote wanaolipa kodi ipasavyo, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuendelea kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari.
Mwenda ametangaza kuwa Julai 1, 2026, TRA itatekeleza maamuzi ya Samia Suluhu Hassan ya kutoa Tuzo ya Rais kwa Mlipa Kodi Bora, ambapo kwa mara ya kwanza tuzo hizo zitatolewa na Rais mwenyewe.
Amesema hatua hiyo inaonyesha namna Serikali inavyothamini mchango wa walipakodi katika kuchochea maendeleo ya taifa, huku akisisitiza kuwa biashara zinapaswa kufanyika katika mazingira yenye utulivu na kuheshimu sheria.
Kwa mujibu wa TRA, maadhimisho ya miaka 30 ya mamlaka hiyo yatakwenda sambamba na hafla ya Tuzo ya Rais kwa Mlipa Kodi Bora, huku taasisi hiyo ikieleza kuwa katika miaka 30 ijayo inalenga kujenga mfumo wa kisasa wa kodi wenye uwazi zaidi, unaorahisisha ulipaji wa kodi na kuhamasisha uzalendo wa kuchangia maendeleo ya nchi.

No comments
Post a Comment