Zinazobamba

MAMBO: BAJETI KUU YA SERIKALI HAIJAONESHA MKAKATI WOWOTE WA KUTATUA CHANGAMOTO ZA VIJANA


*Amesema Serikali imeshindwa kuweka Mazingira rafiki kwa vijana kujikwamua kiuchumi.

*Amesema kuwa asilimia kubwa ya uzalishaji na ukuaji wa uchumi nchini unafanywa na vijana.

Na Mussa Augustine.

Mratibu wa Jukwaa la Vijana Taifa la Chama cha Ukombozi wa Umma(JUVICHA), Masoud Mambo, amesema kuwa vijana nchini ndio waathirika wakubwa wa mchakato wowote wa maamuzi unaofanyika serikalini.

Amesema pia vijana ndio soko kubwa kutokana na uzalishaji mkubwa wanaoufanya, lakini pamoja na umuhimu huo wa vijana katika uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa taifa, bado wamekuwa wakikumbana na changamoto lukuki, kama ambavyo vyama vya siasa, taasisi na makundi mbalimbali vimekuwa vikiwasemea.

Amesema hayo Juni 24, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya CHAUMA, Kinondoni Biafra, na kubainisha kuwa Serikali imeshindwa kutengeneza mazingira rafiki kwa vijana na badala yake imekuwa kikwazo kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa vijana wa Kitanzania. 

Amesema kumekuwepo na sheria, sera na taratibu kadhaa ambazo kimsingi zinamnyima kijana nafasi ya kukua kiuchumi na kupata fursa ya kuingia katika ushindani wa soko la kimataifa.

Aidha, amesema kuwa vijana wa Kitanzania wanakumbwa na changamoto ya ukosefu wa ajira na kupanda kwa gharama za maisha. Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana, Tanzania kati ya vijana milioni moja wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka, 

vijana laki mbili tu ndio huajiriwa kwenye sekta rasmi za umma na binafsi, sawa na asilimia 20, huku vijana laki nane (800,000) waliobaki, sawa na asilimia 80, huingia kwenye sekta zisizo rasmi kama vile kuendesha bodaboda, mama na baba lishe, kuuza matunda, mboga mboga na karanga.

Aidha, amesema kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kupitia bajeti kuu iliyosomwa bungeni jijini Dodoma imeongeza gharama za usajili kwa vyombo vya usafiri, ikiwemo bodaboda, kutoka shilingi elfu tisini na tano (95,000) hadi laki moja na elfu hamsini (150,000), hatua ambayo imetajwa kuwa ni kuwadidimiza vijana kiuchumi.

Aidha, amesema kuwa bajeti hiyo pia haijaonesha mkakati wowote wa kutatua changamoto za vijana kutokana na kwamba Serikali imeshindwa kujenga uchumi unaoweza kutengeneza ajira kwa vijana na badala yake imekuwa ikiendelea kutoa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kama suluhu ya ajira.

Katika hatua nyingine, Mambo amesema kuwa Agosti 12 mwaka huu vijana wa CHAUMA wataungana na vijana wote duniani katika kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani, ambayo ni siku muhimu ya kuongeza uelewa mpana juu ya mchango na changamoto zinazowakabili vijana duniani, maendeleo ya vijana kijamii, kisiasa na kiuchumi, kuhamasisha ushiriki wa vijana katika kufanya maamuzi ya maendeleo, pamoja na kukuza amani, maendeleo na ushirikiano kati ya vijana wa mataifa mbalimbali.

“Uongozi wa Jukwaa la Vijana la Chama cha Ukombozi wa Umma (JUVICHA) umeamua kushiriki maadhimisho haya yatakayofanyika jijini Dar es Salaam tukiwa na kaulimbiu yetu, ‘Vijana, Wakati ni Sasa’, ikiwa na lengo la kuhamasisha vijana kuchukua hatua zitakazotengeneza kesho yao iliyo bora na vizazi vijavyo.”

No comments