Zinazobamba

WAFANYABIASHARA SOKO LA MWANANYAMALA WATAKIWA KUTUMIA VIPIMO VILIVYOHAKIKIWA

Mwenyekiti ushirika wa Soko la Mwananyamala(Mfavesco Ltd) Hassan Madika.

Na Mwandishi Wetu

Wafanyabiashara wa Soko la Ushirika (Mfavesco Ltd) la Mwananyamala wametakiwa kuendelea kutumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo (WMA) ili kutoa huduma sahihi kwa wateja.

Rai hiyo imetolewa leo Mei 20, 2026 na Mwenyekiti wa soko hilo, Hassan Madika, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani, ambapo kitaifa yamefanyika mkoani Dodoma.

Aidha, amesema kuwa wafanyabiashara wa ushirika wa soko hilo wanatumia mizani ambayo inahakikiwa kila mwaka na wataalamu kutoka Wakala wa Vipimo, hali ambayo inawafanya watoe huduma inayozingatia vipimo vinavyotakiwa kutolewa.

“Wakati tunaanzisha ushirika wa soko mwaka 1962, jambo la kwanza kabisa ambalo lipo kwenye katiba ni suala la vipimo. Kipimo ndio kinaweka mahusiano mema kati ya mnunuzi na muuzaji, watafurahiana pale kila mtu anapata haki yake,” amesema.

“Tumesimamia jambo hili kwa kufuata katiba yetu na sheria ya vipimo inayotuongoza, na yeyote atakayetoa vipimo visivyo sahihi anachukuliwa hatua au kufukuzwa sokoni hapo, kwa sababu soko halihitaji mambo ya kubahatisha, na wanunuzi wetu wanafurahia suala la manunuzi.”

Amesema hata magunia yanayotoka mikoani Serikali ilitoa maelekezo yawe na kilogramu 100 tu. Kabla ya hapo, magunia yalikuwa na ujazo wa hadi kilo 200 hadi 300 (Rumbesa), jambo ambalo lilikuwa na athari kubwa kwa wauzaji pamoja na washusha mizigo kuchoka haraka.“Tutaendelea kuwaelimisha watu wajue umuhimu wa vipimo, na wataalamu wa vipimo wanakuja kila mwaka kuhakiki vipimo hapa sokoni, na sisi tunaendelea kuhakiki kila wakati kama wauzaji wanapima kwa ufasaha.”amesema

Nakuongeza “Kuna masoko yamekufa kwa sababu ya kuharibu vipimo. Soko letu ni la ushirika, lina bodi ambayo inashirikiana na wazee wakongwe waliopo hapa sokoni, hivyo kunakuwepo upendo kati ya wauzaji na wanunuzi, ndiyo maana soko letu lipo vizuri,” amesema.

Aidha, amesema kuwa Wakala wa Vipimo huwa wanahakiki vipimo sokoni hapo na kwamba baada ya uhakiki huo viongozi huendelea kusimamia ili huduma iendelee kuwa sahihi.Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara akiwemo Riziki Shangwe ambaye ni mfanyabiashara wa mchele pamoja na Abdunuri Shomari, muuzaji wa samaki, wamesema kwa nyakati tofauti kuwa mizani wanayotumia kutoa huduma ina vipimo sahihi na kuwaomba wafanyabiashara wenzao kuendelea kutoa huduma kwa kuzingatia vipimo sahihi.

“Tuna vipimo sahihi, tunatoa huduma sahihi, naomba wafanyabiashara wenzangu tuendelee kutoa huduma sahihi kwa wateja wetu,” wamesema wafanyabiashara hao.



No comments