SHINGO AONGOZA ZOEZI LA UCHANGIAJI DAMU UKONGA

Mbunge wa Jimbo la Ukonga Bakari Shingo (wa kwanza)akichangia damu wakati wa uzinduzi wa zoezi la uchangiaji damu katika vijawanja vya Pungu Kajiungeni.
*Asema kuna uhitaji mkubwa wa damu mahospitalini.
*Awaomba wananchi kujenga tabia ya kuchangia damu.
Na Musaa Augustine
Mbunge wa Jimbo la Ukonga kupitia chama cha ACT Wazalendo, Bakari Shingo, leo Mei 10, 2026 ameongoza zoezi la uchangiaji damu katika viwanja vya Pugu Kajiungeni vilivyopo jimboni humo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo lililoandaliwa na Ofisi ya Mbunge pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Amana, Afisa Tarafa wa Jimbo la Ukonga, Kheri William, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo, amesema zoezi hilo limesaidia upatikanaji wa damu itakayookoa maisha ya Watanzania.
Aidha, amesema jitihada zinazofanywa na mbunge huyo ni za kipekee kwani ameamua kuwekeza kwa jamii kwa maono makubwa, ikiwemo kutoa mafunzo ya udereva wa magari, pikipiki na bajaji kwa vijana mbalimbali wa jimbo hilo, hivyo ni muhimu afya zao zikahifadhiwa.
“Mhe. Mbunge unafanya mambo ya kipekee sana.Suala la uhitaji wa damu ni kubwa. Dunia nzima wataalamu wamefanya tafiti lakini hakuna zilizoonesha kuwa tunaweza kutengeneza damu mbadala.
Mtu anaweza kukatika mguu akapata wa bandia, lakini huwezi kuchanganya kitu chochote ili kupata damu,hivyo damu hupatikana kwa kuchangia ili kusaidia wagonjwa mbalimbali,” amesema William
Ameongeza kuwa wataalamu wa Benki ya Damu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Amana wamekumbusha kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa damu kutokana na ajali mbalimbali zinazotokea pamoja na wajawazito wanaojifungua kwa upasuaji, hivyo zoezi hilo ni muhimu kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo hilo, Bakari Shingo, amesema bado kuna uhitaji mkubwa wa damu katika hospitali mbalimbali, hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza kuchangia damu ili kuwepo akiba ya kutosha.
Amesema ataendelea kushirikiana na wananchi wa jimbo hilo katika kuwaletea maendeleo pamoja na kushiriki kikamilifu katika masuala ya afya.
“Tusidanganyike, suala la kuchangia damu ni ibada. Halina vyama vya siasa, ukabila wala dini,damu tunayochangia itatusaidia sisi wenyewe,ndugu zetu na rafiki zetu wenye uhitaji wa damu,” amesema Shingo.
Zoezi la uchangiaji damu lilienda sambamba na matembezi ya hisani (jogging) kutoka Mombasa hadi viwanja vya Pugu Kajiungeni, Jimbo la Ukonga, kwa lengo la kuhamasisha jamii kujitokeza kuchangia damu.













No comments
Post a Comment