KIGODA CHA VIJANA TAIFA NLD KUTANGAZA UZINDUZI WA JUKWAA LA MARIDHIANO YA KITAIFA KWA VIJANA
Kigoda cha Vijana Taifa cha Chama cha NLD kinapenda kuutaarifu umma wa Watanzania pamoja na vyombo vya habari kuwa kinatarajia kuzindua rasmi Jukwaa la Maridhiano ya Kitaifa kwa Vijana, jukwaa maalum litakalolenga kuimarisha umoja wa kitaifa, mshikamano wa vijana pamoja na kujenga msingi mpya wa maelewano na maridhiano nchini Tanzania.
Jukwaa hilo litabeba kauli mbiu isemayo.
“MOYO MMOJA, TAIFA MOJA, TANZANIA MOJA KWA MUSTAKABALI WA TAIFA LETU”
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Vijana Taifa ya NLD kilichofanyika leo tarehe 10 Mei 2026 katika ofisi za chama hicho zilizopo Tandika, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Vijana Taifa wa NLD, ndugu Sabra Masanza, amesema kuwa wakati umefika kwa vijana wa Tanzania kuwa mstari wa mbele katika kujenga taifa lenye mshikamano, upendo, amani na maridhiano ya kweli.
Amesema kuwa tofauti za kisiasa, kijamii au kiitikadi hazipaswi kuwa sababu ya vijana wa Tanzania kugawanyika, bali zinapaswa kuwa msingi wa kujifunza kuheshimiana, kusikilizana na kujenga mustakabali wa pamoja wa taifa.
“Maridhiano si udhaifu, bali ni ishara ya ujasiri, subra, hekima na uzalendo wa kweli. Vijana wa Tanzania wana wajibu wa kuunganisha taifa letu na kuweka mbele maslahi mapana ya nchi yetu kuliko tofauti zetu,” amesema Sabra Masanza.
MALENGO YA JUKWAA HILO NI PAMOJA NA.
Kuanzisha mazungumzo ya wazi na jumuishi kati ya vijana wa vyama mbalimbali vya siasa nchini, kukuza utamaduni wa uvumilivu wa kisiasa, mshikamano na kuheshimiana miongoni mwa vijana, pamoja na kukutanisha makundi mbalimbali ya vijana wenye mitazamo tofauti kwa lengo la kujenga umoja wa kitaifa.
Jukwaa hilo pia litaendesha kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha amani, maridhiano na uzalendo kwa vijana kupitia kauli mbiu ya.
“MOYO MMOJA, TAIFA MOJA, TANZANIA MOJA KWA MUSTAKABALI WA TAIFA LETU”
Aidha, jukwaa hilo litakusanya maoni, ushauri na sauti za vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania kwa lengo la kuwasilisha mapendekezo yao kwa Serikali pamoja na wadau wa kisiasa kuhusu namna bora ya kuimarisha umoja wa kitaifa.
Kigoda cha Vijana Taifa NLD pia kimetangaza kuwa kitaandaa Kongamano la Kitaifa la Vijana litakalowakutanisha vijana kutoka vyama vyote vya siasa, asasi mbalimbali pamoja na makundi ya kijamii kwa lengo la kujadili mustakabali wa taifa na nafasi ya vijana katika kujenga Tanzania yenye umoja na matumaini mapya.
Kupitia jukwaa hilo, vijana watahamasishwa kuwa mabalozi wa maridhiano, amani na mshikamano katika maeneo yao nchini kote.
Kigoda cha Vijana Taifa NLD kinaamini kuwa nguvu ya taifa lolote huanzia kwa vijana wake, na kwamba Tanzania yenye umoja, amani na maendeleo ya kweli inaweza kujengwa kupitia mshikamano wa vijana wenye maono ya kizalendo.
Tunatoa wito kwa vijana wote wa Tanzania, viongozi wa kisiasa, taasisi mbalimbali pamoja na wadau wa maendeleo kuunga mkono juhudi hizi za kujenga taifa lenye umoja, heshima, maelewano na matumaini kwa kizazi cha sasa na kijacho.
IMETOLEWA NA.
Sabra Masanza
Mwenyekiti wa Vijana Taifa – NLD
Dar es Salaam, Tanzania
Simu: 0688 869 393
Tarehe: 10 Mei 2026

No comments
Post a Comment