IZO MOTOR'S COMPANY LTD Yazindua Betri Mpya
*Dotto Magari apewa ubalozi wa kutangaza betri hizo.
*Betri hizo hazitumii maji bali zinatumia draya.
*Zina uwezo wa kudumu kwa muda mrefu.
Na Mussa Augustine.
Kampuni ya IZO MOTOR'S COMPANY LTD leo imezindua bidhaa mpya ya betri ijulikanayo kama “Izo Battery”, ambayo haitumii maji kwa ajili ya kuchaji na ina ubora wa kudumu kwa muda mrefu.
Kampuni hiyo inayopatikana Kariakoo, Narung’ombe na Limumba jijini Dar es Salaam, imesema uzinduzi huo unalenga kutoa suluhisho la upatikanaji wa betri za magari zenye ubora kwa bei nafuu nchini.
Akizungumza leo Mei 12, 2026 wakati wa uzinduzi wa betri hiyo, balozi wa bidhaa hiyo na mwenye ushawishi mkubwa mitandaoni, Dotto Magari, amesema betri hiyo haitumii maji bali inatumia draya, huku mteja anayenunua akipewa waranti ya miaka mitano.
Aidha, amesema kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini, kampuni hiyo ya wazawa imeamua kuwekeza katika utengenezaji wa betri hizo ili kutoa ajira kwa Watanzania pamoja na kukuza uchumi wa nchi.
Ameongeza kuwa kwa sasa wanazo aina mbalimbali za betri katika saizi tofauti zinazokidhi mahitaji ya magari ya aina mbalimbali, huku bidhaa hizo zikipatikana kwa bei nafuu kwa jumla na rejareja.
“Kampuni ya ‘Izo Battery’ imeingia makubaliano na mimi kuwa balozi wake. Kupitia ushirikiano huu naamini bidhaa hizi zitaendelea kuwafikia Watanzania wengi zaidi pamoja na masoko ya kimataifa, huku ubora wetu ukiendelea kujenga imani kubwa kwa watumiaji,” amesema Dotto Magari.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa IZO MOTOR'S COMPANY LTD, Bw. Izo Mahenge, amesema betri hizo zimetengenezwa kwa kiwango cha ubora wa hali ya juu kutokana na ushindani uliopo katika soko.
“Izo Battery zinazalishwa hapa Tanzania. Ni betri bora na imara, na watumiaji wa magari hawatajuta kutumia ‘Izo Battery’ popote walipo,” amesema Mahenge.
Ameongeza kuwa, “Kwenye kiwanda chetu tumeajiri zaidi ya watu 60, na tuna mawakala zaidi ya 70 nchi nzima wanaosambaza betri hizi. Tumekuja na bidhaa tofauti.”





No comments
Post a Comment