CRDB Bank kupata washindi 10 kwenda kuangalia Kombe la Dunia Marekani na Canada
Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Kadi kutoka CRDB Bank Makao Makuu, Karim Tonchage, amesema benki hiyo imepata washindi 10 watakaokwenda kuangalia Kombe la Dunia nchini Marekani na Canada, huku wengine 10 wakijishindia TV Janja za nchi 85.
Akizungumza na vyombo vya habari Mei 12, 2026, katika Makao Makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa droo ya kusaka washindi hao, meneja huyo amefafanua kuwa washindi hao wanatokana na kampeni yao kubwa iitwayo “Fainali Ndiyo Mpango na Tembo Card Visa”.
“Kampeni hii kubwa inawahusisha wateja wanaotumia Tembo Card Visa katika matumizi yao ya kila siku kwa kuchanja, na kadiri unavyochanja ndivyo unavyojiongezea nafasi ya kushinda tiketi ya kwenda nchini Marekani au Canada kushuhudia mashindano ya Kombe la Dunia 2026,” amesema.
Aidha, ameongeza kuwa, “Kampeni hii ilizinduliwa mwezi Machi na imebatizwa jina la ‘Fainali Ndiyo Mpango na Tembo Card Visa 2026’, huku ikitoa hamasa ya matumizi ya kadi na miamala ya kidijitali katika shughuli mbalimbali.”
Baadhi ya Washindi wa TV Janja nchi 85
Pia amesema kampeni hiyo inalenga kupata washindi 20, ambapo washindi 10 watajishindia tiketi za kwenda nchini Marekani na Canada kushuhudia wachezaji wa kimataifa kama Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakizitumikia timu zao za taifa za Argentina na Ureno.
Amesema washindi wengine 10 watajinyakulia TV Janja za nchi 85 kila mmoja pamoja na king’amuzi kitakacholipiwa na CRDB Bank ili waweze kutazama mubashara mashindano ya Kombe la Dunia 2026 wakiwa nyumbani pamoja na familia zao.
Amefafanua kuwa kati ya washindi 10 wa tiketi za kwenda kuangalia Kombe la Dunia 2026, washindi sita watakwenda nchini Marekani na washindi wanne watakwenda nchini Canada.
Amehitimisha kwa kusema kuwa katika droo ya kwanza ya mwezi Aprili walipatikana washindi wanne walioshinda tiketi za kwenda nchini Marekani kuangalia Kombe la Dunia, huku washindi watatu wakijishindia TV Janja za nchi 85.

No comments
Post a Comment